Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 05 26Article 539941

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Leseni zinavyowaweka  huru wachimbaji wadogo

“MTU yeyote (kukundi, kampuni au ushirika) anaweza kupatiwa leseni ya kuchimba madini. Sharti ni kwamba awe Mtanzania kuanzia umri wa miaka 18. Hata hivyo, leseni hazitolewi kwa maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria,” anasema Ofisa Madini kutoka Kitengo cha Leseni mkoa wa kimadini Kahama, Marwa Getenyi.

Ofisa huyo alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika semina iliyoandaliwa na taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na kuendeleza wachimbaji wadogo (FADev) katika mkoa huo wa kimadini wa Kahama.

Anataja baadhi ya maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kuchimba madini kuwa ni eneo la jeshi, eneo la kihisitoria, eneo la makazi ya watu, eneo la vyanzo vya maji, hifadhi ya misitu na kadhalika.

Ofisa huyo anafafanua kwamba kuna aina mbili za leseni; ya kufanya utafiti wa madini na nyingine ni ya uchimbaji na uchenjuaji madini.

Anasema leseni hizo hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini namba 14 ya Mwaka 2010 ambayo inatoa ridhaa ya kuchimba, kutafiti, kuuza au kununua madini.

Kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha sheria hiyo, hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kufanya shughuli zozote za kutafuta na kuchimba madini bila idhini ya mamlaka husika (kwa maana ya kupata leseni).

Gitenyi anakiri kwamba utoaji wa leseni umesaidia sana kupunguza migogoro kwa wachimbaji wadogo na hivyo anatoa rai kwa yeyote anayetaka kutafiti au kuchimba madini ahakikishe anapata leseni na siyo kujichimbia holela.

Anasema kuwa zipo adhabu zitokanazo na uvunjifu wa sheria zilizowekwa na pia wapo waliokuwa wakivamia kwenye hifadhi za misitu na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba waliobainika wamechukuliwa hatua.

Adhabu kwa mtu anayekwenda kinyume cha sheria, kwa mujibu wa kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo ni kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja endapo atapatikana na hatia.

Hata hivyo, Getenyi anasema kuwa wachimbaji wadogo, licha ya kupatiwa leseni baadhi yao bado wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha.

Anasema ni muhimu sana wakishapatiwa leseni, wajitambulishe ili kupata ushauri toka kwenye mamlaka za serikali za mitaa na vijiji katika maeneo yao.

Getenyi anasema kisheria eneo analotakiwa kumiliki mchimbaji mdogo ni lisilozidi hekta 10 (ekari 25) ambapo, mbali na kuomba leseni kwa shughuli za uchimbaji, mhusika anatakiwa pia kuchunga suala zima la kutunza mazingira.

Anasema wachimbaji pia wanawajibika kurudisha faida kwa jamii kwa kutoa mchango (CSR) kwa vitu kama ujenzi wa zahanati katika eneo husika, ofisi za kutolea huduma za jamii, uletaji wa miundombinu ya maji na kusaidia sekta ya elimu.

Waziri wa Madini, Doto Biteko anasema serikali inatoa leseni kwa wachimbaji wadogo na kwamba wanatakiwa kuzitumia ili kujipatia maendeleo katika shughuli zao kwani zinawawezesha kuchimba madini bila kubughudhiwa.

Biteko anasema kuwa wilaya ya Kahama ambayo kimadini inatambulika kama mkoa inashika nafasi ya tatu kitaifa katika uzalishaji wa dhahabu. Mkoa unaoongoza ni Geita ukifuatiwa na mkoa wa Mara. Hivi karibuni, aliyekua mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (sasa Mkuu wa Mkoa wa Tanga) alikaririwa akisema anaamini Mara ina madini mengi kuliko Geita.

Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha mwaka jana mkoa wa kimadini wa Kahama ulizalisha tani 4 na kilo 260 za dhahabu ambazo zimeuzwa kwa shilingi bilioni 478 serikali imepata kodi ya shilingi bilioni 79.

Kamishana wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma anawataka watafiti wa madini waliopatiwa leseni kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na serikali pale wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka migogoro isiyokuwa na tija kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha anasema kuwa sekta ya wachimbaji wadogo inakuwa kwa kasi hasa kwa kuzingatia kwamba zamani walikuwa hawapo kwenye mpango rasmi unaotambulika na serikali na zaidi walijikita kujitafutia riziki tu.

Lakini sasa anasema uchimbaji mdogo umeonekana kuwa na tija kwa taifa na wanapewa leseni kwa kadri wanavyohitaji.

Macha anasema Tanzania hivi sasa imeanza kufaidika kutoka kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu tofauti na zamani ambapo macho yalielekezwa zaidi kwa wachimbaji wakubwa.

Anasema Kahama ina wachimbaji wadogo zaidi ya 10,000 na kwamba leseni zimetolewa kwao na kwamba zinaendelea kutolewa, hivyo anawataka wachimbaji wadogo kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima na kufuata sheria.

Cosmas Ndembuke ambaye ni Meneja wa mgodi mdogo wa Kasi Mpya uliopo Mwazimba, kata ya Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama anakiri kwamba hatua ya wachimbaji wadogo kupewa leseni badala ya kujichimbia holela inasaidia sana kuepuka na migogoro.

“Wachimbaji wakija bila leseni watachimba hovyohovyo na sehemu hiyo inakuwa hatarishi na kuzusha migogoro kwani watakuwa hawana viongozi wa kuwasimamia. Lakini ukiwa na leseni unachimba kadri ya mpaka wako na unakuwa huru hata ulipaji wa kodi unakuwa ukienda vizuri kwa kuwa na msimamo,” anasema Ndembuke.

Ndembuke anasema kuwa wao wamejiunga kwenye kikundi na kupata leseni na sharti la kujiunga kwenye kikundi chao ni kumiliki duara la kuchimba au kuchenjua na mitambo ya kisagia mawe maarufu hapa karasha (crasher).

Emanuel Masanja, Meneja wa mgodi mdogo wa Tambarare uliopo kata ya Segese katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama anasema kuwa mgodi huo ulianza rasmi mwaka 2019 baada ya kupatiwa leseni na kuwa eneo lao wanalolimiliki kihalali.

“Ninashukuru kupata leseni katika eneo letu. Tumelipa kodi zinazohitajika serikalini lakini changamoto tuliyonayo bado uchimbaji unaonekana kuwa mgumu kwani bado hatukopesheki kwenye taasisi za fedha ili kuongeza mitaji yetu itakayotusaidia kupata vifaa vya kisasa vya kuchimbia na gharama za utafiti,” anasema.

Ofisa programu na mtafiti kutoka taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na kuendeleza wachimbaji wadogo (FADev), Evans Rubara, anasema walianza rasmi kazi hiyo mwaka mwaka 2019 baada ya kuona bado sekta ya wachimbaji wadogo iko nyuma.

“Hata mimi ninaamini leseni ni njia mojawapo ya kuondoa au kupunguza migogoro kwenye jamii. Labda swali la kujiuliza ni kweli maeneo wanayopatiwa leseni yana dhahabu na yamefanyiwa utafiti wa kutosha?” Anahoji na kuongeza kwamba hofu yake ni wahusika wasije wakawa wanapoteza muda wao na nguvu zao.

Anasema kuwa baadhi ya wachimbaji wa madini wanasema kuwa maeneo waliyonayo yamefanyiwa utafiti na kutambulika kuwa kuna madini lakini tatizo ni kwamba hawafahamu ni katika kina gani watayafikia madini baada ya kuchimba.

Ni katika muktadha huo anatamani kuona serikali na wadau wakiumuza vichwa ili kuwasaidia wachimbaji wadogo katika eneo hilo la utafiti ili isiwe kazi ya kutumia jasho jingi na faida kidogo au bila faida kabisa.

Hata hivyo, anaishukuru serikali kwamba sera zilizopo zinawapatia unafuu mkubwa wachimbaji wadogo, hususani katika suala la ulipaji kodi.

Join our Newsletter