Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 18Article 558166

Habari za Biashara of Saturday, 18 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Maagizo mapya ya Waziri Mbarawa kwa Bandari kuhusu mapato

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuwa waziri na kusema atahakikisha utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) unaongeza mapato hadi kufi kia zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwaka.

Alibainisha hayo jana alipofanya ziara katika mamlaka hiyo na kuzungumza na menejimenti ya TPA ambapo aliwapa maagizo kadhaa ya kutekeleza ili kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo ikiwemo kuanzisha mfumo wa mkataba wa utendaji.

“Katika mambo ninayoyatilia mkazo kwenu ni utendaji. Wanaonifahamu watakumbuka niliwahi kuanzisha performance contract (mkataba wa utendaji) na nina kusudia kuanzisha tena hapa mfumo huo,” alisisitiza.

Alifafanua kwamba mkataba huo utakuwa unapima utendaji wa kila mfanyakazi wa mamlaka hiyo na kwamba atakayebainika kulegalega hatosita kumuacha nyuma.

Alisema anaamini kupitia mkataba huo utendaji wa bandari utaongezeka maradufu na mapato yanayokusanywa kila mwezi yataongezeka na kufikia zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwaka.

Aidha, aliitaka mamlaka hiyo kusimamia vyema miradi yake ili ikamilike kwa wakati na kusisitiza kuwa bado miradi mingi ya TPA haifanyi vizuri.

“Nimekuja hapa na kukagua mradi huu wa kuboresha bandari ya Dar es Salaam wa ujenzi wa gati kuanzia namba sifuri hadi saba. Mradi uko vizuri na umefikia asilimia 99.

Lakini bado nasisitiza muongeze nguvu katika eneo hili la miradi ili ikamilike,” alisema.

Alisema magati hayo ambayo ukarabati wake hadi kukamilika unagharimi Sh trilioni moja, yanaboreshwa ili kupokea meli na mizigo mikubwa zaidi.

Alisema gati namba sifuri (maarufu kama Roll-in Roll-out –Roro) linapanuliwa na kuongezwa kina ili kuongeza meli kubwa zaidi kuleta mizigo ya magari.

Mbarawa pia alitoa agizo la kuhakikisha wafanyakazi wa mamlaka hiyo wanaboreshewa maslahi ili wafanye kazi kwa weledi na kuiwezesha bandari hiyo kukuza uchumi wa nchi.

“Bandari ni injini ya uchumi wa nchi yetu. Sasa kila mmoja anatakiwa kuwajibika kwa hali na mali lakini pia wafanyakazi nao wanatakiwa kuangaliwa maslahi yao,” alisema Mbarawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi alisema amepokea maagizo hayo na atayafanyia kazi. Alisema mamlaka hiyo imekuwa ikifanya vizuri kimapato ambapo mwaka wa fedha 2020/21 ilikusanya Sh bilioni 910, sawa na asilimia 111 ya lengo.

Alisema miaka iliyopita bandari hiyo ilikuwa inakusanya kuanzia Sh bilioni 600 hadi 780 na mwaka 2019/20 ilikusanya Sh bilioni 900.

Aidha, alisema kwa mwezi Agosti pekee bandari hiyo imekusanya Sh bilioni 417, tofauti na mwezi kama huo mwaka jana ambao ilikusanya Sh bilioni 404.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na utendajikazi wa wanyakazi wa mamlaka hiyo wa ushirikiano na kujutuma. “Niweke wazi tu kuwa nilipokuja hapa nilikuwa na hofu kwamba sitapokelewa vizuri.

Lakini hali ni tofauti, nimepewa ushirikiano mzuri na kwa kweli tunachapa kazi,” alisisitiza Hamissi.