Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 10Article 556603

Habari za Biashara of Friday, 10 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Maazimio manne yaliyotolewa na Bunge kuhusu bei ya Mahindi

Maazimio manne yaliyotolewa na Bunge kuhusu bei ya Mahindi Maazimio manne yaliyotolewa na Bunge kuhusu bei ya Mahindi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali leo itatoa taarifa kuhusu utaratibu wa kununua mahindi katika mikoa inayozalisha zao hilo kwa wingi.

Wakati huo huo, Bunge limeazimia mambo manne likiwamo la serikali kuongeza fedha kununua mahindi kwa wakulima, vituo vya kununua mahindi viwe jirani na wakulima, mipaka ifunguliwe ili wafanyabiashara wauze mahindi nje ya nchi au wanunue kutoka huko na pia bei za pembejeo zipungue.

“Serikali imesikia kilio cha wabunge na kesho itatoa taarifa juu ya utaratibu wa kununua mahindi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inatumia kama chakula na zao la biashara,” alisema Majaliwa bungeni jana.

Bunge liliridhia maazimio manne baada ya Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga (CCM) kutoa hoja ya kuomba lijadili hoja ya dharura kuhusu hali ya ununuzi wa mahindi nchini.

Alisema serikali inatakiwa kutoa Sh bilioni 100 kununua mahindi kwa kuwa Sh bilioni 14 zilizotolewa awali hazikutosha.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda akichangia hoja hiyo, alisema ni kweli bei ya mahindi ni ndogo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Ruvuma, Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe na mingine.

“Uzalishaji wa mahindi katika misimu miwili ni mara mbili ya mwaka jana, lakini kumekuwa na changamoto ya soko katika nchi jirani,” alisema.

Profesa Mkenda alisema serikali inafanya jitihada kutafuta masoko katika nchi jirani kama Zambia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini ili kuyasafirisha kwenda kuuzwa huko.

Alisema Bodi ya Mazao Mchanganyiko imeingia mkataba wa kuuza mahindi tani 100,000 na pia imefungua kituo cha mauzo Nairobi, Kenya ambapo pia yatauzwa Sudan Kusini.

Alisema pia mazungumzo yamefikiwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya kununua mahindi tani 20,000 kitika kuhakikisha mahindi yana nunuliwa kutoka maeneo mbalimbali.

Profesa Mkenda alisema wizara hiyo imezingatia maelekezo ya CCM ya kuzungumza na Hazina ili kupatikana fedha za kununua tani 100,000 za mahindi kwa wananchi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayozalisha mahindi kwa wingi.

Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Daniel Chongolo kiliagiza serikali iongeze fedha kununua tani 100,000 za mahindi na kusogeza vituo vya kununulia mahindi karibu na wakulima.