Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 07 15Article 547042

Habari za Biashara of Thursday, 15 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Machinga 500 K’koo kuhamia Machinga Complex

Machinga 500 K’koo kuhamia Machinga Complex Machinga 500 K’koo kuhamia Machinga Complex

WAFANYABIASHARA wa Soko Kuu la Kariakoo lililoungua Julai 10, mwaka huu, wanameanza kuhamisha bidhaa zao katika Soko la Machinga Complex, Ilala mkoani Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao waliohamisha bidhaa ni wale wa maduka ya mzunguko katika soko hilo (vigoli) ambao hawakuathirika na moto uliounguza soko hilo.

Akizungumza na HabariLEO, Makamu Mwenyekiti wa Wajasiriamali Wadogo (Machinga) katika Soko Kuu la Kariakoo, Steven Lusinde alisema jumla ya wafanyabiashara 99 wa vigoli tayari wameshaanza kuhamisha bidhaa.

“Wameanza kuanzia asubuhi kuhamisha bidhaa, hawa wa vigoli ambao maduka yao yanazunguka soko la Kariakoo na mali zao hazijaungua. Hapa wafanyabiashara 99 wanahamisha bidhaa zao kwenda Soko la Mchinga Complex na bado zoezi hilo linaendelea,” alisema Lusinde.

Lusinde alisema kwa upande wa Machinga utaratibu wa kuwaratibu unaendelea ambako jumla ya Wamachinga 500 wanatarajiwa kuhamishwa katika Soko la Machinga Complex.

“Tangu jana tumeanza kufanya utaratibu wa kuangalia taarifa zao na kuwaratibu hivyo zoezi bado linaendelea na litakapokamilika watahamishiwa katika maeneo hayo,” aliongeza kiongozi.

Kwa upande wake, Ofisa wa Soko la Kisutu, Titus Teesphory alisema tayari wafanyabishara wa soko la Kariakoo wameshafika katika soko hilo na kazi ya kuratibu linaendelea.

“Bado tunaangalia utaratibu wa kuwaweka tunachofanya wakija tunachukua taarifa zao kama vile namba ya duka lake au kibanda, bidhaa anazouza na namba zao za simu.

“Idadi kamili bado sijaipata kwa sababu wanaendelea kuja tangu asubuhi hata sasa hivi bado wanakuja na hawa wanaokuja ni kwa ajili ya kuwaratibu tu kwani bidhaa zao ziliungua hivyo wanajipanga upya ndio waanze biashara.

“Kazi yetu sisi ni kuhakikisha kwanza wanapata maeneo watakapojipanga kuanza biashara watakuja,wafanyabishara wanaokuja hapa ni wa mbogamboga na maduka,” alisema Teesphory.

Kuhama kwa wafanyabishara hao ni kutokana na agizo alilolitoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ambaye baada ya soko lao kuungua aliagiza kuhamia katika masoko mengine.

Makalla pia aliagiza wafanyabiashara ambao wako katika soko dogo kuendelea kufanya kazi kutokana na soko hilo kutoathiriwa na moto.