Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 19Article 572662

Habari za Biashara of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Madini ya kinywe kujenga viwanda Ulaya, Marekani

Madini ya kinywe kujenga viwanda Ulaya, Marekani Madini ya kinywe kujenga viwanda Ulaya, Marekani

Baada ya majaribio na vipimo kadhaa vya maabara, Kampuni ya Volt Resources inayochimba madini ya kinywe (graphite) mkoani Mtwara inajipanga kwenda kujenga viwanda Marekani na Ulaya vitakavyozalisha bidhaa zitokanazo na madini hayo.

Volt, kampuni yenye makao makuu yake Australia, ni mchimbaji mkubwa wa madini ya kinywe, ikiwa na maeneo kadhaa inayoendelea kuyatafiti nchini.

Utafiti huo uliofanywa kwa miaka kadhaa sasa, umetoa matokeo chanya katika Mgodi wa Bunyu uliopo mkoani Mtwara na sasa uwekezaji mkubwa wa kuanza uzalishaji unatarajiwa kufanywa, ndani na nje ya Tanzania.

Taarifa ya kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Australia (ASX) inasema majaribio 170 ya betri za simu za mkononi ilizofanya yameonyesha matokeo mazuri yanayothibitisha madini hayo kuwa na sifa zinazotakiwa.

“Tunafurahia kuwa majaribio ya kinywe inayopatikana Bunyu inafaa kwa utengenezaji wa betri na vifaa vya kuhifadhia umeme. Sasa tutaanza upembuzi yakinifu wa kiwanda cha kuzalisha betri Ulaya na Marekani,” alisema Mkurugenzi Matendaji wa kampuni hiyo, Trevor Matthews katika taarifa yake.

Alisema watafanya tathmini na sampuli za teknolojia tofauti pamoja na watumiaji waliokuwa katika mazungumzo nao miezi kadhaa iliyopita kwa ajili ya utekelezaji, hususan upande wa magari ya umeme.

Hata hivyo, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kampuni hiyo haitasafirishaji madini hayo yakiwa ghafi kwa kuwa sheria mpya ya madini inazuia hilo, bali watayaongezea thamani kabla ya kusafirishwa kama ambavyo sheria inataka.

“Sheria inawabana kusafirisha madini ghafi, lakini si lazima kusafirisha bidhaa ya mwisho, watayaongezea thamani hapa na wanaruhusiwa baada ya hapo kusafirisha kwenda nje kwa ajili ya kutengenezea bidhaa.”

Biteko alisema kampuni hiyo kuanza uchimbaji kutakuwa na manufaa ya ujenzi wa viwanda na Serikali kuongeza mapato mapya ya kikodi, tozo na ajira kwa watu watakaoajiriwa katika miradi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiRasilimali, Racheal Chagonja alisema endapo viwanda hivyo vya betri vikianzishwa nchini vitatoa fursa kubwa kwa Watanzania kunufaika na madini hayo kuliko vikianzishwa nje ya nchi.