Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 04 28Article 535717

Habari za Biashara of Wednesday, 28 April 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Madini yaongoza mapato fedha za kigeni

Madini yaongoza mapato fedha za kigeni Madini yaongoza mapato fedha za kigeni

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema katika kipindi cha mwaka jana, sekta ya madini ilikua kuliko sekta nyingine huku ikiongoza pia kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Profesa Msanjila aliyasema hayo jana kwenye ufunguzi wa kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini ambalo linajumuisha wajumbe kutoka Makao Makuu, Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa, Kamishna wa Kazi, Viongozi wa Tughe ngazi ya Taifa, Mkoa na Tawi la Tume ya Madini.

Alisema tangu kuanzishwa kwa Wizara ya Madini, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kwa kasi na kusisitiza kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha mchango huo unafikia asilimia 10 ifikapo 2025.

Alisema Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za madini ikiwamo kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini kwa wachimbaji wadogo wa madini, ushirikishwaji wa Watanzania kwenye sekta ya madini, wawekezaji kutoa huduma za jamii kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini.

Akielezea mafanikio ya sekta ya madini tangu kuanzishwa kwa Wizara ya Madini, alisema kasi ya utoaji wa leseni imeongezeka ambako katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi, 2021, imetoa leseni za madini 8,709 na uanzishwaji wa ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa na maofisa migodi wakazi ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni uanzishwaji wa masoko ya madini 39 na vituo vya ununuzi wa madini 50 ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wanapata masoko ya uhakika ya madini yao, kuimarika kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini kupitia ujenzi wa ukuta wa Mirerani na kuimarisha ulinzi kwenye viwanja vya ndege na mipakani na usimamizi dhabiti wa mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akizungumza kwenye ufunguzi wa baraza hilo, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuaminiwa na kumteua kuendelea kuisimamia Tume ya Madini.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Yahya Samamba akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa lengo la kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi lilikuwa ni kujadili changamoto za utendaji kazi pamoja na kuzipatia ufumbuzi, kupitia bajeti kwa mwaka wa fedha 2021-2022 na kupewa mafunzo mbalimbali.

Join our Newsletter