Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 08 31Article 554590

Habari za Biashara of Tuesday, 31 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Majaliwa aagiza magogo kupigwa mnada

Majaliwa aagiza magogo kupigwa mnada Majaliwa aagiza magogo kupigwa mnada

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuyakusanya na kuyapiga mnada magogo aina ya mkulungu yaliyopo katika kijiji cha Wachewaseme wilayani Kaliua, mkoani Tabora.

Ametoa agizo hilo jana katika ziara yake mkoani humo alipokagua miradi mbalimbali ya maendeleo na hifadhi ya msitu wa akiba.

Amesema kuwa magogo hayo 8,000 yaliyokamatwa na serikali ya kijiji yauzwe ili walipwe wakusanyaji na fedha zingine zipelekwe Serikali Kuu.

Katika ziara yake, Majaliwa alitembelea eneo la Pori la Akiba la Igombe na kushuhudia magogo yaliyokatwa bila kufuata utaratibu wa kupata vibali.

Waziri Mkuu amewaasa wananchi kuachana na tamaa ya kutaka utajiri wa haraka na kwamba watakao kamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya dola.

Katika hatua nyingine ameagiza Mamlaka ya Usmamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuongeza ulinzi katika eneo hilo ili kulinda wanyama wanaokatiza na wasisite kuwakamata wote wanaofanya ujangili.

Wakati huo huo, Majaliwa amewapa miezi miwili viongozi wa mkoa huo pamoja na wilaya kukagua ujenzi wa kituo cha afya ili kikamilike pamoja na kuwalipa vibarua fedha zao.

Akikagua mradi wa jengo la kituo cha afya cha Usinge, Majaliwa alisikitishwa ujenzi huo kutokamilika kwa wakati.

Amesema kituo hicho kimegharimu Sh. milioni 628 zilizotolewa na serikali, lakini mpaka sasa hakijakamilika.

Amesema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa viongozi wake, kuhakikisha pande zote za nchi kujenga vituo vya huduma za afya ili Watanzania wapate huduma.

Majaliwa amesema serikali imeongeza vituo vitatu vya afya vya Usinge, Uyowa na Mwongozo na vyote vimejengwa kwa gharama ya kati ya Sh. milion 400 hadi 500.

"Nashangaa Mkoa wa Tabora, saruji ipo, mchanga upo na mawe yanapatikana kwa nini ujenzi haujakamilika," alisema Majaliwa.