Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 18Article 558217

Habari za Biashara of Saturday, 18 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Majaliwa aonya hujuma mkakati utatuzi tatizo mafuta ya kula

Majaliwa aonya hujuma mkakati utatuzi tatizo mafuta ya kula Majaliwa aonya hujuma mkakati utatuzi tatizo mafuta ya kula

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaonya baadhi ya wananchi katika Mkoa wa Kigoma, wanaohujumu zao la kimkakati la michikichi kwa kuchoma moto na kulisha mifugo.

Amesema huo ni uhujumu uchumi na kuwahakikishia Watanzania kuwa kilimo hicho muda si mrefu kitamalizia upungufu wa mafuta ya kula baada ya mbegu iliyofanyiwa utafiti aina ya TENERA kuanza kutoa matunda ndani ya miaka miwili na nusu.

Akizungumza juzi na wananchi wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo yake kuhusu kuendeleza michikichi katika shamba la ekari 6,000 la Gereza la Kwitanga wilayani Kigoma, Waziri Mkuu alisema serikali itawachukulia hatua kali wale wote wanaofanya hujuma dhidi ya zao hilo.

“Nimepita katika shamba la michikichi la Gereza la Kwitanga ambalo wamepanda zao hilo tangu mwaka jana lakini wananchi wamewasha moto na kuunguza shamba lote karibu asilimia 80. Sasa nawaonya hilo ni zao la kimkakati na tumeweka sheria kali sana isije ikakuangukia “

Waziri Mkuu alisema mbegu hiyo ya Tenera imeonyesha ina uwezo wa kuzalisha mafuta tani tano mpaka sita kwa hekta moja tofauti na mbegu ya zamani inayozalisha wastani wa tani 1.6 kwa hekta.

 

Pamoja na hujuma hiyo, Waziri Mkuu alisema kutokana na mafanikio ya mbegu hiyo, aliwataka wakulima wa zao hilo katika Mkoa wa Kigoma kuiondoa kwa awamu aina ya michikichi iliyopandwa kwa kutumia mbegu ya zamani inayoanza kuzaa baada ya miaka saba.

“Wakulima wa michikichi mmeliona hili shamba. Tumepanda mbegu ya Tenera mwaka 2019 lakini mpaka sasa ni miaka miwili na tayari imeanza kutoa matunda, hivyo nawaomba mpande hii mbegu mpya katika mashamba yenu huku mkitoa kwa awamu ile mbegu ya zamani aina Dura,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alipongeza Gereza la Kwitanga kwa kuamua kulima ekari 6,000 za michikichi kwa kuwa utakuwa mradi mkubwa wa jeshi hilo ambao utasaidia kuongeza mapato na kujitegemea.

Aliagiza uongozi wa gereza hilo kuongeza uzalishaji wa mbegu za Tenera na kuwapatia bure wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka gereza ili walime michikichi kwa kutumia mbegu ya kisasa.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Geofrey Mkamilo, alisema miongoni mwa maelekezo waliyopokea kutoka kwa Waziri Mkuu ni kuzalisha mbegu bora aina ya Tenera ambayo mpaka sasa wahazalisha zaidi ya mbegu milioni 3.5 na kuzigawa bure katika taasisi na halmashauri nane za mkoa huo.

Alisema maelekezo mwingine hao watu wanaopatiwa mbegu hizo wanapaswa kuzitunza na kuhakikisha zinaota kwa kuwa gharama za kuzalisha miche ni kubwa. Alibainisha kuwa mche mmoja gharama halisi ni Sh. 1,000.

Mkurugenzi huyo alisema katika maeneo mbalimbali waliyopita, wamegundua baadhi ya miche inaliwa na mifugo na mingine inachomwa moto kitu ambacho kinasababisha hasara kwa serikali.

Dk Mkamilo alisema miche kuliwa na wanyama au kuchomwa moto ni jambo  lisilokubalika kwa sababu linaweza kurudisha nyuma mkakati wa nchi wa kuzalisha mafuta ya kula.