Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 23Article 559150

Habari za Biashara of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Makampuni 20 kutoka Uganda yanayotarajiwa kuwekeza Tanzania

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim

KAMPUNI 20 za nchini Uganda zinajipanga kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbali mbali katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Homa nchini humo hadi Tanga.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim alisema hayo Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio ya ziara ya taasisi hiyo nchini Uganda hivi karibuni.

Abdulrahim aliwaeleza waandishi habari kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imetoa Dola za Marekani 500,000 ili kuwajengea wajasiriamali wazawa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana na mradi huo.

Katika ziara hiyo, ATOGS na na Taasisi ya Sekta Binafsi Uganda (PSFU) walisaini mkataba wa ushirikiano katika miradi ya gesi na mafuta.

Abdulrahim alisema mkataba huo utaziwesha ATOGS na PSFU kushiriki kikamilifu katika mradi mkubwa wa kusafirisa mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

“Katika ziara yetu, tumebaini kuwapo kampuni 20 za Uganda zinazokuja Tanzania kufungua kampuni na sisi sekta binafsi tutashirikiana na wadau wote ili Waganda wanapokuja Tanzania kuwekeza, wasisumbuke,” alisema.

Abdulrahim alisema walichokifanya kina lengo la kulinda viwanda na wazalishjaji kwa kutokuwahusisha watu wa nje kwa vitu vinavyowezekana kufanywa na Watanzania na Waganda.

Mkataba ulisainiwa nchini Uganda na unahusisha mambo kadhaa ikiwemo namna ambavyo wazawa wa pande zote mbili wanavyoweza kunufaika na fursa mbalimbali katika ujenzi wa bomba hilo.

“Fursa zilizopo ndani ya huu mradi ni nyingi. Huu ndio muda sahihi wa kuzishughulikia changamoto zinazozuia biashara kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine ili kuweka mazingira mazuri wakati mradi utakapoanza,” alisema

Alisema makubaliano yamefikiwa kati ya programu ya kuwanoa wajasiriamali wadogo na wa kati ya Benki ya Stanbic na ATOGS kuwanoa wajasiriamali wa Uganda ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa na fursa zitakazojitokeza.

Kwa mujibu wake, Mwenyekiti wa PSFU, Dk Elly Karuhanga aliishukuru ATOGS kwa wazo la kuanzisha ushirikiano huo na kwamba utasaidia kuhakikisha wananchi wa pande mbili wananufaika na fursa zitokanazo na mradi huo.

Balozi wa Uganda nchini, Richard Kabonero alisema mradi huo ni haki ya Watanzania na Waganda kushiriki, na kwamba yapo maeneo maalumu ya fursa 13 yaliyotengwa kwa ajili ya Waganda na 17 kwa wajili ya Watanzania.