Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 11Article 542173

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mauzo bidhaa nje yaongezeka

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioisha, mauzo ya bidhaa nje yameongezeka kwa asilimia 12.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema jana kuwa, katika mwaka unaoishia Aprili 2021, thamani ya mauzo ya bidhaa iliongezeka kufikia Dola za Marekani bilioni 6.35 kutoka Dola za Marekani bilioni 5.67 kipindi kama hicho mwaka 2020.

Dk Mwigulu alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

"Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia na zisizo asilia ikiwemo dhahabu, madini mengineyo, bidhaa za maua na mbogamboga pamoja na bidhaa za viwandani,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ilipungua kwa asilimia 7.4 kutoka Dola za Marekani bilioni 8.75 katika mwaka unaoishia Aprili 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 8.11 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

"Hali hiyo ilitokana na kupungua kwa uagizaji wa baadhi ya bidhaa kufuatia kuimarika kwa uzalishaji katika viwanda vya ndani, hususan bidhaa za ujenzi kama vile marumaru, nondo na saruji,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema katika mwaka unaoishia Aprili 2021, urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje uliimarika kufikia nakisi ya Dola za Marekani milioni 1,177.2, ikilinganishwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 1,443.6 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Dk Mwigulu alisema kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa kulichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu na bidhaa za maua na mbogamboga sambamba na kupungua kwa thamani ya uagizaji wa mafuta na vyombo vya usafiri.

Alisema katika mwaka unaoishia Aprili 2021, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma ilifikia Dola za Marekani bilioni 8.5 kutoka Dola za Marekani bilioni 9.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

"Upungufu huo ulitokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii, ikiwa ni matokeo ya hatua zilizochukuliwa na mataifa mengine duniani ili kupunguza kasi ya maambukizi ya Uviko -19 (Ugonjwa wa Virusi vya Korona), hususan kuzuia safari za kimataifa,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje ilifikia Dola za Marekani bilioni 9.3, ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 10.5 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Mwiguku alisema mapato yatokanayo na huduma yalipungua kutoka Dola za Marekani bilioni 3.89 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2020, hadi Dola za Marekani bilioni 2.20 Aprili 2021.

Join our Newsletter