Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 08Article 541651

Habari za Biashara ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mauzo bidhaa za Tanzania EAC zaongezeka

Mauzo bidhaa za Tanzania EAC zaongezeka Mauzo bidhaa za Tanzania EAC zaongezeka

MAUZO ya bidhaa kwa Tanzania kwenda katika nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeongezeka katika mwaka 2019 na takwimu za awali za mwaka 2020.

Thamani ya bidhaa zinazotoka Tanzania na kuuzwa kwenda nchi wanachama imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 444.3 mwaka 2018 hadi dola milioni 674.4 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 51.8.

Aidha, thamani ya manunuzi ya bidhaa kutoka nchi wanachama iliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 302.7 mwaka 2018 hadi dola za Marekani milioni 329.2 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 8.7.

Aidha, takwimu za awali za mwaka 2020 zinaonesha mauzo ya Tanzania kwenda nchi wanachama ni dola za Marekani milioni 812.55 wakati manunuzi kutoka nchi wanachama yalikuwa dola milioni 324.31.

Takwimu hizo zimeoneshwa katika Taarifa ya Biashara na Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2019 iliyoridhiwa na Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao Desemba mwaka jana.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akiwasilisha bungeni makadilio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2021/2022.

Alisema baadhi ya bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni mahindi, mchele, chuma, marumaru, karatasi na saruji. Tanzania imeendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kunufaika na fursa zilizopo katika Mtangamano wa Afrika Mashariki.

Alieleza kuwa hayo ni baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki na kubainisha kuwa thamani ya manunuzi baina ya nchi wanachama iliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 2,835.9 mwaka 2018 hadi dola milioni 3,175.8 mwaka 2019 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 12.

Alisema thamani ya mauzo ya bidhaa baina ya nchi wanachama iliongezeka kutoka dola za marekani milioni 3,145.2 mwaka 2018 hadi dola za milioni 3,162.8 mwaka 2019, ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 0.6.

Balozi Mulamula alisema Septemba 2020, wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la EAC uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Alisema katika mkutano huo ulijadili maombi ya Uingereza ya kufanya majadiliano ya Mkataba rasmi wa Biashara na Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Alisema Baraza la Mawaziri la Kisekta lilikubaliana na pendekezo la majadiliano hayo na kuagiza nchi wanachama kushiriki majadiliano kwa pamoja kama jumuiya.

“Aidha, ilipendekezwa Serikali ya Uingereza isogeze mbele muda wa kukamilisha majadiliano kutoka Desemba 31, mwaka jana hadi 31 Desemba, 2021 ili kutoa muda kwa nchi wanachama kufanya mashauriano ya ndani,” alieleza.

Join our Newsletter