Uko hapa: NyumbaniBiashara2022 01 09Article 584395

Habari za Biashara of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Meli kubwa yatia nanga gati mpya Mtwara

Meli kubwa yatia nanga gati mpya Mtwara Meli kubwa yatia nanga gati mpya Mtwara

Meli kubwa ya kwanza kutia nanga kwenye gati jipya katika Bandari ya Mtwara yenye urefu wa meta 199.9 imewasili bandarini hapo kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe kupeleka nchini India.

Meli hiyo imeletwa na Kampuni ya Ruvuma Coalmine inayojulikana kwa jina la Star Fighter ikitokea nchini Pakistani yenye uwezo wa kubeba tani 59,000 ya makaa ya mawe kutoka bandarini hapo kupeleka India ikiwa ni meli ya kwanza kutia nanga kwenye gati hilo jipya ambalo serikali imewekeza Sh bilioni 157.8 katika ujenzi wa gati hiyo.

Akizungumza jana katika tukio hilo la ujio wa meli bandarini hapo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdillah Salim alisema kuwa ujio wa meli hiyo na kutia nanga kwenye gati hilo jipya ni matokeo ya serikali katika kuboresha bandari hiyo pamoja na maendeleo ya Kusini mwa Tanzania.

“Ujio wa meli kama hii kwetu sisi ni faraja kwa sababu biashara inaongezeka na kwa ujumla tunafanya kazi na Watanzania wengine wote wa Kusini wanapata ajira kwa hiyo sisi tumefurahi kuja kwa meli hii,” alisema.

Aliongeza: “Tusingeweza kupata uzito huu wa tani hizi 59,000 kwa hiyo maboresho ya hapa na ujenzi huu wa bandari mpya ndio umesababisha meli hii iweze kufunga hapa… tunawahakikishia wa Kusini na Watanzania kwa ujumla kuwa tuko tayari kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maendeleo yanakuwepo.”

Mkurugenzi wa huduma za Meli na Utekelezaji wa shughuli za kibandari kutoka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Abdallah Mwingamno alisema ni mara ya kwanza kuleta meli kubwa kwenye gati hilo jipya lililojengwa kwa fedha za serikali.

“Itapakia mzigo huu ndani ya siku saba kulingana na vifaa tulivyokuwa navyo kwa sasa kwa hiyo haya ni maendeleo makubwa kabisa ambayo serikali imeyafanya na inaendelea kuyafanya. Kwa maboresho haya tunaamini kwamba hii biashara ya kimeli ya kibandari inaendelea na tunaingiza nchi kwenye ushindani,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya alisema ujio wa meli hiyo ni fursa kubwa kwa watu wa Mtwara. Alisema wanafarijika kwa ajili ya kukuza uchumi wa biashara kwani uwekezaji huo wa gati hilo jipya bandarini hapo umekuwa kivutio kikubwa watu kuleta meli zao kwa ajili ya kuchukua bidhaa mbalimbali mkoani humo.

“Tunaishukuru sana Kampuni ya Ruvuma Coalmine kwa jinsi ambavyo mmeamua kuja kuleta meli yenu kubeba mzigo na bandari hii ya Mtwara. Lazima itumike kwa ajili ya manufaa ya sisi wana Mtwara na Taifa. Tutaendelea kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amewekeza Mtwara,” alisema Kyobya.