Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 08 23Article 553186

Habari za Biashara of Monday, 23 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Mkumbo aiongezea majukumu TANTRADE

https://ippmedia.com/sw/biashara/mkumbo-aiongezea-majukumu-tantrade https://ippmedia.com/sw/biashara/mkumbo-aiongezea-majukumu-tantrade

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuwa kituo cha kibiashara kinachotoa taarifa, takwimu sahihi na huduma bora za kibiashara ndani na nje ya nchi ili kukuza na kuendeleza biashara nchini.

Alitoa agizo hilo juzi jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANTRADE.

Prof. Mkumbo aliitaka bodi hiyo kusimamia ipasavyo majukumu muhimu ya TANTRADE ikiwamo kuanzisha kanzi data yenye taarifa za kibiashara na kufanya utafiti, ili kujua ni bidhaa gani zinazalishwa kwa wingi nchini.

“Nataka kuona TANTRADE inakuwa kimbilio kwa wanyabiashara katika kuwaunganisha wazalishaji, wasindikaji wafanyabiashara kutoka maeneo ya uzalishaji na walipo wateja wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi kwa kutoa taarifa na takwimu sahihi pamoja na huduma bora za kibiashara,” alisema Prof. Mkumbo.

Pia, aliitaka bodi hiyo kuhakikisha TANTRADE inaongeza ubunifu katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya kimtandao ya biashara inayolenga kuongeza upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kibiashara kwa urahisi, ili kuwezesha upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.

“Bodi hii pia inatakiwa kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na sekta binafsi katika kuelimisha na kuhamasisha uboreshaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini, upatikanaji wa masoko, uendeshaji wa biashara, kujenga uelewa juu ya usafirishaji wa bidhaa hizo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kufikia soko la ndani, kikanda na kimataifa,” alisema Prof. Mkumbo.

Aidha, aliielekeza bodi hiyo kutekeleza jukumu la msingi la bodi katika kutengeneza mkakati wa kufikia malengo ya taasisi na kusimamia utekelezaji wake kwa kutoa ushauri ndani na nje ya vikao vya bodi.