Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 11Article 562558

Habari za Biashara of Monday, 11 October 2021

Chanzo: ippmedia.com

Mkurugenzi CRDB apewa tuzo

Mkurugenzi CRDB apewa tuzo Mkurugenzi CRDB apewa tuzo

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amechaguliwa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu Bora wa mwaka 2021 katika Tuzo ya Uongozi Bora katika mashirika.

Nsekela alipokea tuzo hiyo kwenye hafla ya mwisho ya orodha ya watendaji bora 100 wa Tanzania mwishoni mwa wiki katika hafla ya kila mwaka.   Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, lengo ni kutambua na kusherehekea mafanikio ya mtu binafsi na mashirika. Tuzo hizo ziliandaliwa na Taasisi ya 'Eastern Star Consulting' kwa lengo la kuhamasisha maofisa kuanzia ngazi ya chini kwenye mashirika makubwa.   Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, alielezea kujitolea kwa serikali katika kuwezesha uwekezaji na biashara, akisema itaongeza ujasiri wa wafanyabiashara wa Tanzania kushindana katika soko la kimataifa.

Alisema serikali inafanyika kazi baadhi ya sera ili kuboresha urahisi wa kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi na kupunguza uwepo wa serikali katika biashara hizo.   Alisema kulikuwa na pengo kubwa la ustadi kati ya wahitimu wa Kitanzania huku waajiri wakilaumu taasisi za juu za elimu kwa kuzalisha wataalam wasiokidhi vigezo, huku wakisahau kuwa mafunzo kazini yanamjenga na kupanua uwelewa zaidi kwa mfanyakazi.   Alisema tuzo zilizotolewa zitaongeza juhudi kwa maofisa na watendaji wa mashirika katika maeneo yao ya kazi kwa kuwa wataona juhudi na maarifa kwa kuwa yanathaminiwa kwa tuzo kama hizo.   Wengine waliopata tuzo ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi ambaye aliibuka wa pili kwa kura akifuatiwa na Jared Awando wa Shirika binafsi la Bima la ICEA.   Aidha, kipengele kingine katika tuzo hizo, Friedrick Nshekanabo kutoka CRDB alichaguliwa kuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu Bora, huku Christina Manyenye kutoka KCB Benki aliibuka mshindi wa Ofisa Biashara Mkuu.   Katika hotuba yake wakati akipokea tuzo hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu Bora, Nsekela alisema tuzo hiyo si kwa juhudi zake peke yake bali pia imechangiwa na wafanyakazi wenzake wa CRDB.   "Haya ni matokeo ya kufanya kazi kama timu, lakini upendo na urafiki baina yetu… tuzo hii naitoa kwa familia yangu, mke na watoto wangu kwa kunipa utulivu, bila utulivu kichwani ni ngumu kufanya vizuri," alisema Nsekela.