Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 03Article 540712

Habari za Biashara of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Maganda ya nanasi  yanavyogeuzwa  unga wa mikate

Maganda ya nanasi   yanavyogeuzwa   unga wa mikate Maganda ya nanasi  yanavyogeuzwa  unga wa mikate

KIPINDI cha msimu wa nanasi wafanyabiashara wengi wamekuwa wakimenya na kuuza vipande vipande kati ya shilingi 100 hadi mia 400 kutegemea ukubwa.

Katika msimu wake biashara hii imekuwa ikifanya vizuri hususan kwenye maeneo ya watu wengi kama sokoni, stendi, hospitali na kwingineko.

Wakati huo huo, kipindi hicho huzalishwa takataka nyingi za maganda ya nanasi ambapo mfanyabiashara asipokuwa msafi zinaweza kutoa harufu na kuvuta inzi ambao husambaza magonjwa ya mlipuko.

Lakini kumbe maganda hayo ya nanasi ambayo huonekana ni takataka yanaweza kuongezewa thamani kwa kuanikwa na kusagwa kisha kutoa unga ambao unatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuchanganya na unga wa nfano wakati wa kuoka mikate ama kuwekwa kwenye chai kwani yana virutubisho vingi kwa afya ya binadamu.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeonyesha teknolojia hiyo wakati wa Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Sayansi na Teknolojia ya Chakula Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Lilian Kaale anasema wametumia ubunifu katika kuongeza thamani na kupunguza upotevu kwenye matunda pamoja na mboga za majani.

Anasema katika utafiti walioufanya waligundua kuwa kwenye nanasi wanapotengeneza juisi huharibika baada ya siku chache hivyo kabla haijaharibika wakaona watengeneze bidhaa nyingine ambayo inaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika.

Anasema juisi inapotengenezwa wakati wa kuchujwa kuna mabaki ya nanasi ambayo huwa na virutubisho vingi hivyo huanikwa na kusagwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

“Kwa kawaida watu wengi hutupa kama uchafu mabaki hayo lakini kama unataka kutafuta madini chuma na kashamu kwa ajili ya mifupa inapatikana huko,” anasema.

Kwa maelezo ya Dk Kaale pia kuna nyuzinyuzi ambazo ni nzuri kwa ajili ya kusafisha utumbo mpana na kuzuia kupata kansa.

“Sasa badala ya kutupa haya maganda sisi tunayachukua na kuyaanika kwa ajili ya kutengeneza unga. Huo unga una virutubisho vingi sana,” anasema.

Anasema kwenye Ndaki yao hiyo pia wanahamasisha kula matunda pamoja na mboga za majani.

Katika uhamasishaji huo wanatengeneza unga wa mabaki hayo ya nanasi pamoja na mboga za majani ili kuwawezesha wale wasiopata matunda kirahisi kuyapata au kwa wale wasiopenda kula matunda au mboga za majani.

Anasema unga huo wanaoutengeneza wa mabaki ya nanasi na mboga za majani wanakuwa wamelenga makundi matano ambayo ni watoto, wajawazito, wazee, wanafunzi wa bweni ambao wengi wao wameathirika kwa asilimia 80 kwa sababu hawali vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.

Wanafunzi hao wanaporudi nyumbani wanakuwa na vidonda vingi mdomoni.

“Kwa hiyo wanafunzi wanapokwenda shuleni ukichukua huo unga ukawaambia wakati unapokula ugali chukua kijiko kimoja weka kwenye supu na kama anakunywa uji vile vile watapata virutubisho wanavyovikosa,” anasema na kuongeza kuwa hata watoto wadogo wanaweza kuwekewa kwenye supu au uji.

Anasema kwenye kiungo cha chai kuna tangawizi na mchachai halafu wanaweka na unga huo wa nanasi lengo ni kulenga kila mtu apate virutubisho hivyo.

“Kiungo hicho cha chai kinanukia vizuri sana na mtu hatajua kama imewekwa mabaki ya nanasi kwani lengo kubwa la utafiti huo ni uhamasishaji wa kula matunda,” anasema.

Lakini pia kwenye Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu idara hiyo ilionyesha bidhaa mbalimbali zilizoongezwa thamani na mabaki ya nanasi ikiwemo mkate.

Anasema kwenye mkate huo umetengenezwa kwa kutumia mabaki hayo ya nanasi kisha kuchanganywa na viazi lishe kwa lengo la kuhamasisha ulaji wa matunda.

“Kwa ujumla tumetumia bidhaa nne tofauti kuanza kuhamasisha ulaji wa matunda. Nanasi kama nanasi lina virutubisho vingi tumetengeneza juisi tukasema mtu anaweza kunywa lakini yale mabaki tunayotaka kutupa ndiyo yana virutubisho vingi sana na tumeyatumia kufanya uhamasishaji wa ulaji wa matunda,” anasema.

Dk Kaale anasema baada ya utafiti huo wameweza kujenga wajasiriamali wa aina nne tofauti. Mjasiriamali wa kwanza ni yule mkulima wa nanasi ambaye anajua kuna soko, wa pili ni yule ambaye anatengeneza juisi akijua anaweza kuchukua mananasi yaliyolimwa.

“Lakini tumeweza kuzalisha wajasiriamali wengine ambao watakuwa wanajihusisha kukusanya hayo mabaki ya mananasi na kuyakausha na kutengeneza unga hivyo unapokwenda dukani unasema nataka ‘supplement’ ya matunda.

“Tunaweza tukatengeneza moduli nyingine za matunda sio nanasi pekee lengo letu ni kuona hii teknojia inakwenda kwenye matunda mengine yote na mboga za majani ili watu waweze kula matunda,” anasema.

Mjasiriamali mwingine ni yule anayezalisha ambapo unga huo utauzwa dukani lakini pia mwingine anaweza kutumia kutengeneza mkate na biskuti.

Anashauri serikali kuendeleza kuona ni kwa jinsi gani inaweza kuchukua ubunifu na utafiti unaofanywa na taasisi za elimu za juu ili kuweza kuwafikishia wananchi.

“Kwa mfano, kwa hatua hii tayari tumeongeza thamani kwenye haya matunda, tumepunguza upoteaji wa haya matunda, tumezalisha kazi na tumeongeza uchumi wa nchi.

“Ombi langu kwa serikali ni kuona ni kwa jinsi gani inaweza kutumia hii moduli tuliyoitumia hapa tuweze kuitumia na kufikishia jamii,” anasema.

Akizindua Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu UDSM yenye kaulimbiu ya Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Jamii nchini Tanzania’, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivitaka vyuo vikuu nchini kuweka utaratibu wa kufanya utafiti kisha kuonesha matokeo ya utafiti huo kama ilivyofanya UDSM ili kuimarisha uhusiano wa karibu baina yao na jamii.

Katika maadhimisho hayo Majaliwa alishauri wataalamu kutumia utafiti wanaoufanya kwani ni suluhisho la changamoto mbalimbali.

Alisema kwa kuwa na utaratibu huo kunaweza kuwa moja ya sababu ya kuvutia wafadhili na hatimaye kupanua wigo wa ushirikiano wa ndani na nje ya nchi kwenye utafiti.

Pia aliwataka wenye viwanda pamoja na wafanyabiashara katika sekta mbaliombali zinazotegemea ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia kuunga mkono jitihada za vyuo vikuu za kufanya utafiti badala ya kutegemea serikali pekee kutenga bajeti hiyo.

Katika maadhimisho hayo Majaliwa alikiri kujifunza mambo mengi ikiwemo namna ya kuzalisha samaki aina ya kambale pamoja na teknolojia ya jiko linalotumia mionzi ya jua na hivyo kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hatua inayochangia uharibifu wa mazingira.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye anasema kupitia utafiti chuo hicho kina wajibu wa kutatua matatizo yanayokabili jamii.

“Ni wazi kuwa mwanataaluma asiyefanya utafiti ana hatari ya kuwa na hali ya mwalimu wa shule ya msingi au sekondari, chuo kikuu ambacho ni makini hakiwezi kuwavumilia wanataaluma wa aina hiyo,” anasema.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anasema maonyesho hayo yanatoa fursa ya wadau wa utafiti kufahamu tafiti zinazofaa na zenye upungufu ili kuondoa upungufu huo.

Pia anasema yanatoa fursa kwa taasisi nyingine za elimu kujifunza kwani ni fursa ya kubadilishana uzoefu kutoka taasisi za elimu ya juu.