Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 05 04Article 536314

xxxxxxxxxxx of Tuesday, 4 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtaji wa 400,000/- wakifanyia makubwa kikundi cha kilimo

KILIMO ni uchumi, kilimo ni ajira, kilimo ni chakula na Waswahili wanasema, jembe halimtupi mkulima. Ni katika muktadha huo, akinamama wa Kijiji cha Kome, Kata ya Bwasi, Musoma Vijijini mkoani Mara, walianzisha kikundi cha Jipe Moyo kwa ajili ya kilimo.

Katibu wa kikundi hicho, Deborah Isaack, anasema wanaendesha bustani za matikiti maji, nyama, vitunguu na kabeji na kwa kuwa wanalima kando ya Ziwa Victoria wanatumia maji ya ziwa hilo kumwagilia mazao yao.

“Lakini pia tunaendesha kilimo kinachotegemea mvua kwa mazao ya mahindi, mihogo, maharage na alizeti ambalo ni zao jipya huku kwetu, ila linastawi vizuri,” anasema Deborah.

MWANZO WA KUKINDI Katibu huyo anasema, Jipe Moyo kilianzishwa miaka saba iliyopita kikiwa na wanachama 12, baada ya yeye kuwahamasisha wanawake wenzake lakini sasa kina wanachama 35.

“Tulichangishana fedha, tukapata Sh 400,000 ambazo tulizitumia kununua mbegu za matikiti maji na vifaa vingine. Baada ya mavuno ya kwanza tulipata Sh 500,000 ingawa lengo lilikuwa ni kupata milioni moja,” anasema.

Anasema, walitumia fedha hizo kulima eka moja ya mahindi na mihogo, lakini pia wakapanua kilimo cha bustani kwa kuongeza mazao ya nyanya, vitunguu na kabeji.

Hatua hiyo ya kuongeza mazao, anasema ilisaidia kuendelea kutunisha mfuko wao hadi kuanza kulima alizeti.

“Wadau wa kilimo akiwamo mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, walitusaidia jembe la kukokotwa na ng’ombe, lakini pia kila mwaka mbunge amekuwa akitusaidia mbegu za mahindi, mihogo, mtama na alizeti,” anasema.

Anasema, shirika lisilo la kiserikali la Project Concern International (PCI) nalo lime kuwa msaada mkubwa kwao kwa kuwapa mashine ya kumwagilia bustani na kwamba limeahidi kuwapa mashine ya kukamua mafuta ya alizeti.

Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma nayo iliwakopesha Sh milioni 12 kwa awamu mbili kwa ajili ya kuendelea kuimarisha kikundi chao ambacho anasema kimekuwa mfano mzuri katika Kata ya Bwasi.

Aidha, anasema, wamejiwekea utaratibu kwa kila mwanachama kununua hisa kuanzia moja hadi tano, moja ikinunuliwa kwa Sh 2,000, na kwamba mkopo kwa kila mwanachama unategemea hisa zake na anaweza kukopeshwa kuanzia Sh 100,000 hadi 150,000.

MIPANGO YA BAADAYE Deborah anasema, kikundi cha kina mipango mingi, ikiwamo kuongeza hisa za mfuko katika kukopeshana, kuotesha miti ya mbao na ufugaji wa nyuki kibiashara.

“Vilevile tunakusudia kuanzisha kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, kama tulivyoahidiwa na PCI,” anasema.

Lingine wanalotarajia kufanya anasema ni kuongeza wanachama hadi kufikia 50 na pia kununua mashamba yatakayomilikiwa na kikundi ili kuachana na mtindo wa kukodi wanaotumia sasa.

“Tumedhamiria kujikomboa kiuchumi na tayari tuna zaidi ya Sh milioni 10 benki tangu tuanzishe kikundi chetu, ,” anasema.

KIKUNDI CHA MFANO Ofisa Kilimo wa Kata ya Bwasi, Alex Mihambo, anasema Jipe Moyo kimewafanya wakazi wengine wa Kijiji cha Kome kuanzisha vikundi vya kilimo, na sasa katika kijiji hicho kuna vikundi 15.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vincent Anney anasema, yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake, wanaendelea kushawishi wanavijiji wa Musoma vijijini kuanzisha vikundi kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Join our Newsletter