Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 17Article 571951

Habari za Biashara of Wednesday, 17 November 2021

Chanzo: IPPmedia

Mwinyi ataka biashara ya pamoja Afrika

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali  Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka nchi za Bara la Afrika kuhakikisha zinafanya biashara ya pamoja badala ya kuelekeza nguvu zaidi nje ya bara hilo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za Afrika, unaofanyika Durban, Afrika Kusini ambapo amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk. Mwinyi alisema kuwa ili kufikia azma iliyokusudiwa, ni muhimu kutekeleza malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambapo katika utekelezaji wake alihimiza haja ya nchi wanachama wa AfCFTA kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto zilizopo, ambazo ni kikwazo kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji.

Alizitaja miongoni mwa changamoto zinazozifanya nchi za Afrika zishindwe kufanya biashara baina yao kutokana na kukabiliwa na vikwazo vingi vinavyosababisha kiwango cha biashara kuwa ndogo baina yao pamoja na ufinyu wa miundombinu kati ya nchi zenyewe, utatanishi uliopo kuhusu viwango vya ushuru, migongano ya sheria na uhaba wa bidhaa zinazozalishwa.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba lengo la mkutano pamoja na maonyesho hayo ya Biashara ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi za Afrika hivyo, kuna kila sababu ya kutiliwa mkazo na kufanyiwa kazi ipasavyo azma hiyo.

Aidha, alieleza kwamba kiwango cha kufanya biashara baina ya nchi za Afrika bado ni kidogo mno na badala yake sehemu kubwa ya biashara inafanywa katika nchi zilizoendelea zikiwamo za Ulaya na Marekani.

Marais na viongozi kutoka nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo walipata fursa ya kueleza mikakati na juhudi zinazochukuliwa na nchi zao katika kuhakikisha suala zima la biashara huria linapewa kipaumbele katika Bara la Afrika ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana huku wakieleza athari za UVIKO 19 zilivyorejesha nyuma hatua hiyo.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo, alieleza utayari kwa nchi hiyo katika kutoa ushirikiano juu ya suala hilo.