Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 21Article 573286

Habari za Biashara of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Neema yashukia wakulima wa Vanilla nchini

Neema yashukia wakulima wa Vanilla nchini Neema yashukia wakulima wa Vanilla nchini

Wakati ikielezwa kuwa vanila ni miongoni mwa mazao yenye soko kubwa duniani na thamani yake inapanda kila kukicha, wakulima wametahadharishwa kuwa kilimo cha zao hilo si kazi nyepesi na kinahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kupata faida.

Wakulima na vijana wenye nia ya kuingia kwenye kilimo hicho wametakiwa kuzingatia masharti yote muhimu yanayoambatana na kilimo cha vanila.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Novemba 21, 2021 Mkurugenzi wa kampuni ya Vanila International Limited, Simon Mkondya amesema kwa kutambua ugumu katika uzalishaji wa zao hilo wameanzisha kijiji maalumu ambacho kilimo cha vanila kitakuwa kinafanyika.

Amesema kijiji hicho kilichopo Njombe kina hali ya hewa inayoruhusu kilimo cha vanila na kuna watalaamu ambao wanafuatilia kwa ukaribu kila hatua katika mashamba yaliyopo kijijini hapo.

“Sio kwamba maeneo mengine kilimo hiki hakiwezekani hapana ila tumefanya utafiti na tukaweka vitu vyote vinavyohitajika kule Njombe tukiamini ni sehemu sahihi zaidi ya kulima vanila ndiyo maana tunawaita wakulima waje.

“Mbegu watapata kwetu, kuna watalaamu kule ambao wanafuatilia zao hili, vanila sio kama mazao mengine ambayo yanachavushwa na wadudu, inahitajika mikono ya binadamu kuchavusha hivi vyote vinafanywa na watalaam wetu, mwisho tunapeleka vanila itakayovunwa kwenye soko la kimataifa,” amesema Mkondya.

Kauli ya Mkondya imekuja kukiwa na shauku kubwa ya vijana kuingia kwenye kilimo hicho baada ya kusambaa taarifa kuwa thamani ya zao hiyo inaweza kufika Sh800, 000 kwa kilo moja.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, Mexico, Madagascar, Indonesia, Uganda, Comoro na Papua New Guinea, ndio waagizaji wakuu wa vanila kutoka Tanzania.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi wa kilimo wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Maua Tanzania (Taha) kutoka Zanzibar, Ally Kamtande Ally alisema mwaka 2020 vanila safi iliuzwa kwa Sh850,000 kwa kilo.