Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 22Article 573442

Habari za Biashara of Monday, 22 November 2021

Chanzo: ippmedia.com

PURA yachimba visima 96 vya kutafuta mafuta

PURA yachimba visima 96 vya kutafuta mafuta PURA yachimba visima 96 vya kutafuta mafuta

PURA imetoa kauli hiyo katika kuelezea mafanikio mbalimbali iliyoyapata katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika. 

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa PURA, Charles Sangweni, kati ya visima hiyo 96 vilivyochimbwa, 59 ni vya nchi kavu, 37 baharini huku visima 44 vilivyogundulika kuwa na gesi asilia, nchi kavu viko 16 na baharini viko 28.

Alisema ugunduzi huo umewezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati hususani kwa kuzalisha umeme viwandani, majumbani na kwenye magari.

“Uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004 kwa upande wa maeneo ya SongoSongo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay, hadi sasa kiasi cha gesi kinachozalishwa kinachangia karibu asilimia 60 ya umeme unaozalishwa hapa nchini,” alisema Sangweni.

Alisema gesi iliyogunduliwa nchi kavu na ile ya kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo trilioni 57.54 ambapo kati ya hizo nchi kavu ni trilioni 10.06 na baharini ni trilioni 47.48.

Sangweni alisema uwapo wa gesi hiyo hususani iliyogunduliwa katika eneo la bahari kuu, kumesababisha serikali kuingia kwenye mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi hiyo kuwa katika hali ya kimiminika.

Alisema utafutaji huo wa mafuta na gesi unafanyika kupitia mikataba ambayo PURA inaingia na kampuni mbalimbali zinazokuja kuwekeza nchini.

“Hii mikataba huwa tunaingiana kampuni kubwa zinazokuja nchini kuwekeza na wanachokitafuta kikipatikana tunakaa na kukubaliana namna ya kugawana,” alisema Sangweni.

"Na kampuni hizi pale zinapokosa kile wanachokitafuta mikataba hiyo imetoa nafasi ya wao kuondoka nchini bila kudai chochote kile na nchi hubaki na taarifa pamoja na takwimu ambazo zinakusanywa wakati wote wa utafutaji.

Sangweni alisema hadi sasa maeneo ambayo tayari wameshayafanyia utafiti ni kilomita za mraba 534,000 ambapo kati ya hizo Km 394,000 zipo nchi kavu na Km 140,000 zipo baharini.