Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 22Article 573331

Habari za Biashara of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rwanda yaanza kuitumia Bandari ya Tanga

Rwanda yaanza kuitumia Bandari ya Tanga Rwanda yaanza kuitumia Bandari ya Tanga

Serikali ya Rwanda imeanza kuitumia Bandari ya Tanga kupitishia shehena ya mizigo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima jana alipokea meli yenye shehena ya mzigo wa malighafi ya kutengeneza saruji iitwayo clinka tani 50,000 itakayoshushwa bandarini hapo na kisha kusafirishwa hadi Rwanda.

Malima alisema kupitishwa kwa mzigo huo ni mafanikio ya uwekezaji wa maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Tanga.

"Kwa mara ya kwanza toka bandari hii iwepo leo tumeweza kupokea shehena kubwa ya mzigo wa tani 50,000 na bado tunatarajia kupokea meli kubwa ya mafuta hivi karibuni hii ni kutokana na maboresho tuliyoyafanya katika bandari yetu" alisema.

Malima alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati mpya inayojengwa katika bandari hiyo meli zitakuwa na uwezo wa kutia nanga jirani na bandari hivyo hata meli kubwa zitatria nanga hapo.

"Niwatake mamlaka ya bandari kuendelea na juhudi za kuitangaza bandari yetu ili tuweze kupokea mizigo mingi lakini na kuinua uchumi wa wananchi na mkoa kwa ujumla" alisema.

Meneja biashara wa kampuni ya saruji ya Prime ya nchini Rwanda, Mvayo Fabrice aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kumaliza changamoto zilizowakabili awali.

"Tumeanza kuitumia Bandari ya Tanga kutokana na urahisi wa uingizaji na utoaji wa mizigo hapo awali tulikuwa na Changamoto na WASAFIRISHAJI lakini kwa sasa tunakwenda vizuri mizigo yetu haichelewi tena" alisema Fabrice.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile alisema, kutokana na maboresho yanayoendelea bandari hiyo inatarajia kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani 750,000 hadi 3,000,000 kwa mwaka.

Alisema kuanza kuongezeka shehena ya mizigo ni mwanzo mzuri kwa bandari hiyo kuanza kufanya biashara kwa ufanisi.

"Hii bandari ina miaka 130 kutokana na msukumo wa serikali pamoja na maboresho yanayofanyika sasa tutaanza kupokea shehena kubwa ya mizigo katika bandari yetu" alisema Ngaile