Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 08Article 562030

Habari za Biashara of Friday, 8 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali, UN kushirikiana kukuza uchumi

Serikali, UN kushirikiana kukuza uchumi Serikali, UN kushirikiana kukuza uchumi

Tanzania imesaini makubaliano ya kuendeleza mpango wa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayotekeleza shughuli katika sekta mbalimbali nchini yatakayoanza Julai 2022 hadi 2027.

Mashirika hayo ya UN takribani 22 yanafanya kazi na serikali kupitia wizara na sekta mbalimbali katika kuiletea nchi maendeleo na hasa kustawisha wananchi wake.

Akizungumza jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Mkutano wa kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema kusainiwa kwa makubaliano kutaisaidia nchi katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake.

Tutuba alisema katika mkutano huo ambao makatibu wa wizara mbalimbali zinazofanya kazi na mashirika hayo wapo kwamba kusainiwa kwake kutasaidia nchi kutekeleza mipango yake ukiwemo wa miaka mitano wa maendeleo.

Alisema makubaliano hayo yamesainiwa ili kuendeleza ushirikiano mwingine utakaoanza mwakani hadi mwaka 2027.

Katibu Mkuu Hazina alisema mkutano huo umetumika pia kufanya tathmini ya makubaliano yaliyofanyika 2016 na utamalizika Juni mwakani, ili kuangalia na kuboresha maeneo ambayo pengine yalisahaulika ili kuingizwa katika makubaliano mapya hayo mapya ya Julai 2022 hadi 2027.

Tutuba alisema miongoni mwa mambo muhimu katika makubaliano ya mpangokazi huo ni pamoja kila wizara kupata rasilimali fedha na rasilimaliwatu ili kutekeleza makubaliano hayo mapya.

Ili kutekelezwa kwa ufanisi, kila wizara itaingiza makubaliano katika sekta husika kwa ajili ya kutekeleza vizuri zaidi ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Katika makubaliano yaliyopita, mashirika ya kimataifa yalichangia kwa kiwango kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi na ndiyo maana Tanzania ilifaulu kuingia katika uchumi wa kati wa chini.

“Hivyo makubaliano hayo, baina ya serikali na mashirika hayo, unalenga kuandaa utaratibu mpya wa kushirikiana katika kuhakikisha nchi inaendelea kukuza uchumi na kustawisha umma kupitia sekta za afya na ustawi wa jamii, ukuaji wa uchumi, demokrasia na utawala bora, haki za binadamu pamoja na jinsia,” alieleza.

Pia majadiliano yameangalia kikamilifu kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika sekta hizo namna gani zimeingizwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26.

Mkutano huo pia uliangalia ni kiasi gani mpango wa maendeleo wa miaka mitano umewainishwa na kuingizwa katika mipango ya mashirika ya UN ndani ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs).

Pia yameangalia kiundani namna gani mpango wa maendeleo ya nchi umezingatia mipango au ajenda mbalimbali za Afrika Mashariki na kikanda ikiwemo Ajenda ya Afrika Mashariki (2050) na Ajenda ya Afrika (2063).

Lakini pia makubaliano hayo yamezingatia Mpango wa Kukuza Uchumi Zanzibar (Mkuza) ambao nao unaelekea ukingoni mwishoni mwa mwaka huu na hivyo serikali hiyo maandalizi yake yanatakiwa kuzingatia makubaliano ya serikali na mashirika na kuyaingiza katika maandalizi ya mpango wake mpya.

Ushirikiano baina ya serikali na mashirika hayo tangu umeanza, ni mkubwa na kwa kiasi kikubwa umechangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi katika miongo miwili ambao ulikuwa kati ya asilimia sita hadi saba.

Ukuaji wa uchumi uliathirika na kuingia kwa Covid-19 ambapo mwaka jana uchumi ulishuka hadi kukua kwa wastani wa asilimia 4.8. Hata hivyo, serikali inafanya jitihada kufufua ukuaji wa uchumi ili ukue kwa asilimia tano.

Hivyo ili kuhakikisha uchumi unakua asilimia tano, ushirikiano na mashirika ya kimataifa ni muhimu ili kusaidia serikali zote mbili katika kutekeleza miradi mikubwa ambayo ni chachu ya ukuaji uchumi na ustawi wa jamii.

Hivyo ili kuendelea kukuza uchumi na kustawisha jamii, makubaliano hayo yanaingizwa katika mpango ya bajeti ambayo ndiyo mpango rasmi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya watu.

Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mratibu Mwakilishi wa mashirika ya UN, Zlatan Milisic alisema makubaliano hayo yataangalia kwa undani mkakati wa umoja wa mataifa katika kutekeleza SDGs 2030.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza malengo endelevu na kuangalia namna serikali inavyotekeleza malengo hayo ndaniya mipango yake ya maendeleo.