Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 08Article 562027

Habari za Biashara of Friday, 8 October 2021

Chanzo: mwananchidigital

Serikali yafuta leseni 175 za wachimbaji madini

Serikali yafuta leseni 175 za wachimbaji Serikali yafuta leseni 175 za wachimbaji

Waziri wa Madini, Dotto Biteko amefuta leseni ndogo 175 za wachimbaji mkoani Kagera ambazo wamiliki wake wanadaiwa tozo za Serikali na zilizokwisha muda wake.

Waziri alisema hayo jana akiwa katika Mgodi wa Sindiketi unaochimba madini ya bati uliopo Kata ya Nyaruzumbura wilayani Kyerwa.

Alitoa agizo hilo baada ya mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate kuomba wachimbaji wadogo katika mgodi huo wapewe maeneo ya kuchimba ili waweze kujiongezea kipato na kuchangia mapato ya Serikali.

Waziri alisema leseni 120 zimeisha muda wake na 55 wamiliki wake walishapata hati ya kulipa tozo za Serikali wanazodaiwa, hivyo akaagiza leseni zote 175 zifutwe na maeneo hayo wapewe wachimbaji wadogo.

“Hao wanaodaiwa tuliwapa siku 90 wakashindwa kulipa, naagiza wanyang’anywe leseni zao na waongezewe muda wa kulipa madeni,” alisema Biteko.

Wakati huohuo, Waziri Biteko alimtaka Meneja wa Madini Mkoa wa Kagera, Lukas Mlekwa kusimamia utoaji wa mikataba kwa wachimbaji wadogo kutoka kwa wenye leseni ambayo haitawafunga kuuza madini yao kwenye soko wakishalipa asilimia 20 ya wenye leseni.

“Nasema hivyo kwa sababu hawa watu wanapata shida, mikataba waliyonayo sasa na wenye leseni inawafunga, wanalazimika kuuza madini kwa mwenye leseni. Sasa hii basi, simamia hili,” alisema Biteko.

Awali, Mlekwa alisema leseni 55 ambazo wamiliki wake wameshapewa hati, zinadaiwa Sh1.1 bilioni.

Mlekwa alisema kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Julai hadi Septemba, ofisi ya madini imekusanya Sh1 bilioni huku madini ya bati yakichangia Sh99.1 milioni sawa na asilimia 132 hivyo kuvuka lengo.

Mmoja wa wachimbaji wadogo katika mgodi wa madini ya bati, Sindiketi Rwekaza alisema kwa sasa bei ya madini hayo inaleta matumaini tofauti na ilivyokuwa mwaka jana. Alisema mwaka jana kilo moja waliuzwa Sh6,000 ila sasa ni kati ya Sh25,000 na Sh36,000.

Kutokana na hilo, Rwekaza alimuomba Waziri Biteko kuendelea kuwatafutia soko zaidi.

“Sisi wachimbaji wadogo tunakushukuru kwa hili alilolifanya waziri lakini tunaomba asiishie hapa, aendelee kututazama kwa jicho la huruma zaidi ili tuzidi kunufaika na shughuli halali tunazozifanya,” alisema.