Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 04Article 561142

Habari za Biashara of Monday, 4 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali yatoa miezi 12 kwa viwanda kubadili chupa za plastiki

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ametoa miezi 12 kwa wenye viwanda vinavyozalisha vinywaji viache kutumia chupa zilizopigwa marufuku.

Alitoa muda huo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa chupa ya moja ya vinywaji vinavyotengenezwa na kiwanda cha Cocacola.

Alivitaka viwanda vizingatie kanuni za mazingira ili Tanzania ifanye vizuri kwenye utekelezaji wa matakwa ya utunzaji mazingira.

Jafo alisema viwanda vingi vya vinywaji vinatumia chupa zisizoendana na matakwa ya mazingira na mara kadhaa serikali imekuwa ikivitaka vizibadilishe.

"Hili ni suala lililopo ndani ya sheria namba 20 ya mwaka 2018 ya utunzaji wa mazingira, hatuna budi kuhakikisha inatekelezwa, nitoe rai kwa wote wenye viwanda hivyo kuhakikisha wanabadilisha chupa za vinywaji hivyo ili ziendane na matakwa ya sheria hii," alisema.

Alikipongeza kiwanda hicho kwa kubadili mwonekano wa chupa ya kinywaji chao kutoka rangi ya kijani na kuwa nyeupe.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka alisema utunzaji mazingira ni jukumu la kila mmoja hivyo lizingatiwe.

Alivihimiza viwanda vya vinywaji vilinde mazingira kwani jambo hilo ni muhimu kwa maisha ya viumbe wakiwemo wanadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Cocacola, Unguu Sulay alisema lengo lao ikifika mwaka mwaka 2025 asilimia 50 ya chupa wanazozizalisha ziwe katika mfumo wa kuwezesha zichakatwe tena na kurudishwa katika matumizi.