Uko hapa: NyumbaniBiashara2022 01 10Article 584617

Habari za Biashara of Monday, 10 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Soda zaadimika mitaani nchini kote

Soda zaadimika mitaani nchini kote Soda zaadimika mitaani nchini kote

KINYWAJI baridi aina ya soda kinachotengenezwa na kampuni za Pepsi na Coca Cola zimeadimika kwa muda sasa tangu Desemba mwaka jana.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLeo katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka kwa wanunuaji wadogo na wakubwa wa kinywaji hicho, umebaini kuwa Desemba mwaka jana soda za Coca Cola zilianza kuadimika na kadiri siku zilivyokwenda Pepsi nayo ikawa inapatikana kwa shida.

Wauzaji wa kinywaji hicho kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa, wafanyakazi wa kampuni hizo wamekuwa wakichukua oda zao kila siku lakini upatikanaji wake ni mgumu.

Mfanyabiashara wa duka la rejareja katika Soko la Vetenary, Dar es Salaam, Robert Ombeni alisema vinywaji hivyo hana dukani kwake tangu juzi na ameshindwa kununua kwa sababu muuzaji wa jumla wa eneo hilo naye hana.

Naye muuzaji wa jumla wa soda katika soko hilo, Ally Mohamed alisema tangu Desemba mwaka jana, kinywaji cha Coca Cola kiliadimika na Pepsi ikawa inapatikana lakini hivi sasa ana wiki nzima hana soda za aina zote kutoka kampuni zote hizo.

“Wafanyakazi kutoka kampuni hizo kama kawaida wanakuja kuchukua oda zetu lakini hatupati vinywaji, hivi sasa ninachouza hapa dukani ni maji pamoja na juisi mbalimbali,” alisema.

Cocacola huuza soda aina za Cocacola, Fanta, Sprite, huku ya Pepsi ikizalisha soda ya Pepsi, Seven Up na Mirinda.

Wafanyabiashara wa maduka na baa katika maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam wameelezea kutopata kinywaji hicho kwa wakati bila kujua sababu ya upoteaji huo ni nini.

Muuzaji wa baa moja iliyopo Buguruni, Tatu Hassan alisema hana kinywaji cha kampuni kutoka Pepsi ama Coca Cola ikiwa ni wiki sasa.

Alisema hawajapewa maelezo rasmi kuwa changamoto ni nini toka kwa wahusika.

Kutoka Dodoma, muuza duka la vinywaji la Imma, eneo la Makole, Imma Tarimo alisema kupotea kwa vinywaji hivyo ni kawaida kwa kila mwisho wa mwaka kutoka na kampuni hizo kubwa kufanya mahesabu ya mwaka.

“Hata ukiangalia soda huwa zinaisha muda wake kipindi hicho, kwa uzoefu wangu hii hali hutokea kila mwaka na inapofika tarehe 15 Januari soko linatengamaa,” alisema.

Naye Khadija Saidi wa Mji Mpya alisema soda zimeadimika pamoja na maji ya kunywa na sigara lakini haelewi sababu kwani wasambazaji wakubwa hawajawapa taarifa zozote.

Sakina Juma muuza duka la vinywaji vya jumla eneo la Bahi Road alisema kuanzia jana soda zimeanza kushushwa kwenye maduka yao ya jumla, lakini mahitaji ni makubwa ya wateja hivyo zinaisha haraka.

HabariLEO iliwasiliana na wasemaji wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na kampuni hizo mbili kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo bila mafanikio.

Imeandikwa na Lucy Ngowi (Dar) na Anastazia Anyimike(Dodoma).