Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 20Article 558544

Habari za Biashara of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Stendi ya Ubungo kuwa kituo cha biashara Afrika Mashariki

Iliyokuwa stendi ya Ubungo kuwa kituo kikuu cha biashara Afrika Mashariki Iliyokuwa stendi ya Ubungo kuwa kituo kikuu cha biashara Afrika Mashariki

Baada ya takriban miaka saba ya majadiliano, hatimaye iliyokuwa Stendi ya Ubungo sasa inabadilishwa kuwa Kituo cha biashara na usafirishaji Afrika Mashariki.

Kituo hicho kikikamilika, pamoja na shughuli nyinginezo, kitakuwa kikipokea bidhaa zote muhimu kutoka China zinazohitajika kwa soko la Afrika Mashariki.

Kituo hicho kitakachogharimu dola za Marekani 114 milioni (zaidi ya Sh264.3 bilioni) kitaanza kujengwa muda wowote kuanzia sasa, baada ya Manispaa ya Ubungo kuruhusiwa kuendelea na mambo kadhaa ya mchakato wake.

Akizungumza kwenye kikao kilichojadili utekelezaji wa mradi huo juzi, Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mradi huo ulitakiwa kuwahi kwani manufaa yake ni makubwa kwa wananchi na Serikali.

“Mradi huu utaongeza mapato ya halmashauri, hivyo kuiwezesha kutekeleza miradi yake ya maendeleo. Tumejiridhisha na uwezo wa mwekezaji, kampuni ya Linghang Group kutoka China…Balozi wetu wa China, Mbelwa Kairuki amefuatilia na kusema ana uwezo mkubwa na anafanya vizuri kule. Malizieni hatua zilizobaki ili mwezi ujao utekelezaji uanze,” alisema.

Profesa Kitila aliikumbusha halmashauri kuachana na urasimu wa aina yoyote kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa, kwani utulivu wa kisera na kisheria ndio utakaosaidia kuvutia wawekezaji zaidi. Mpango wa kubadilisha matumizi ya eneo ilipokuwapo Stendi ya Ubungo, ulianza mwaka 2014 baada ya iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kusaini mkataba wa kutathmini uwekezaji wa jiji la biashara, usalama na ujenzi wa China City, kituo kitakachokuwa kinaingiza bidhaa kutoka China kwa ajili ya nchi zote za Afrika Mashariki.

Mwaka 2015, jiji lilisaini mkataba wa kujenga kituo hicho cha biashara utakaodumu kwa miaka 45, lakini lilipovunjwa, ukahamishiwa Wilaya ya Ubungo ambayo inaenda kuutekeleza kwa miaka 15, huku kukiwa na uwezekano wa kuuhuisha.