Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 20Article 572926

Habari za Biashara of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

TAKUKURU kuchunguza mgodi Mererani

TAKUKURU kuchunguza mgodi Mererani TAKUKURU kuchunguza mgodi Mererani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ameigiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa wizi wa madini kwenye mgodi wa serikali Mirerani, mkoani Manyara.

Ametoa agizo hilo wakati akizindua Mfumo wa Maombi ya Ajira Serikalini kupitia simu za mkononi, jijini Dodoma jana.

Amesema kuna wizi mkubwa wa madini unaofanyika katika mgodi huo na taarifa hizo siyo siri kwani zimeenea katika mkoa wote wa Arusha kuhusu namna gani wizi huo unafanyika na rushwa imetamalaki katika eneo hilo.

“Sasa niwaagize Takukuru, kwa kuwa yupo hapa Mkurugenzi wa Uchunguzi, ninawapa wiki mbili ili mwende mkafanye uchunguzi kuhusu kile kinachoendelea Mirerani kwenye mgodi unaomilikwa na serikali ili kutambua kila kinachoendelea na wizi mkubwa ambao unaendelea kwa taarifa ambazo zimeenea mitaa ya Arusha na mkoa wa Manyara,” amesema Mchengerwa.

Pia ameagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi kuhusu taarifa za uwapo wa ubadhirifu mkubwa wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru kufuatilia suala hilo ili kujua kila kitu kinachoendelea kwa kuwahoji wahusika ili kujiridhisha na taarifa hizo ambazo zimeenea mitaani.

Amesema serikali imepeleka fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali nchini na aliwataka Takukuru kufuatilia jambo hilo ili fedha za miradi zilizopelekwa na Rais Samia Suluhu Hassan zikatoe matokeo chanya.

“Agizo langu ni kwamba, kila kiongozi wa Takukuru awe ni kamanda wa wilaya, kamanda wa mkoa, watapimwa kwa namna ambavyo watasimamia matumizi ya fedha na kuleta matokeo chanya, kila mmoja wetu atapimwa kwa namna ambavyo anakwenda kusimamia matumizi ya fedha ambazo serikali imetoa,” amesema Mchengerwa.

Amewakumbusha TAKUKURU kuwa jukumu lao kubwa siyo kwenda kupambana na rushwa tu, bali kuzuia ili serikali itimize matakwa na malengo yake iliyokusudia kwa Watanzania, hivyo akawataka maofisa wa taasisi hiyo wa wilaya zote nchini kufuatilia taarifa ya fedha zilizoingia na matumizi yake kwa wakandarasi ambao wanatekeleza miradi hiyo ili itoe matokeo chanya.