Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 26Article 544333

Habari za Biashara of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

TARI kugawa mbegu bora za michikichi kwa wakulima

TARI kugawa mbegu bora za michikichi kwa wakulima TARI kugawa mbegu bora za michikichi kwa wakulima

Mkurugenzi wa TARI Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, aliyasema hayo juzi wakati taasisi hiyo ilipokuwa inatoa elimu kwa maofisa kilimo wa maeneo yote ya Wilaya ya Kyela ambayo yanafaa kwa kilimo cha chikichi.

Alisema walifikia uamuzi huo kwa lengo la kuzalisha chikichi kwa wingi ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta unaolikabili taifa kwa sasa pamoja na kuwainua wananchi kiuchumi.

“Chanzo kikuu cha tatizo la uhaba wa mafuta nchini ni ukosefu wa malighafi za kutosha kwa ajili ya kuzalisha mafuta, sasa serikali imeamua kumaliza tatizo hilo kwa kuwekeza kwenye kilimo cha mazao yanayosaidia upatikanaji wa malighafi hiyo na ndio sababu nasi tumeamua kuzalisha mbegu za chikichi hapa wilayani Kyela ili kutimiza azma hiyo ya serikali,” alisema Dk. Bucheyeki.

Alisema kitalu hicho kitasaidia kupanua kilimo cha zao hilo katika mwambao wa Ziwa Nyasa ambako imebainika kwamba zao hilo linaweza kustawi vizuri.

Alisema miche hiyo itasambazwa kwa wakulima ili wapanue mashamba yao ya chikichi na kwamba baada ya miche hiyo kuanza kutoa matunda, suala la uhaba wa mafuta nchini litabakia kuwa historia.

Mratibu wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Dk. Emmanuel Chilagani, alisema kwa kuanzia wamepanda mbegu 41,000 ambazo endapo zitaota zote watapata miche 41,000 na zisipoota zote wanakusudia kupata miche isiyopungua 27,000.

Alisema miche hiyo wataigawa bure kwa wananchi wa Wilaya ya Kyela na maeneo yote ya mwambao wa Ziwa Nyasa na kwamba elimu wanayoitoa kwa maofisa kilimo itasaidia miche hiyo kwenda kutunzwa ipasavyo.

“Hii miche itatosha kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 220, kwahiyo tunawashauri wakulima wa wilaya hii ya Kyela na maeneo yote ya mwambao wa Ziwa Nyasa wachangamkie fursa hii,” alisema Dk. Chilagani.

Naye mtafiti wa michikichi kutoka TARI, Beata Paul, alisema wakulima wengi wa Wilaya ya Kyela wamekuwa wakitumia mbegu za asili ambazo uzalishaji wake hauna tija kubwa kama ilivyo kwa miche ya kisasa na chotara.

Alisema mbegu za kienyeji ambazo wakulima huzitumia huchukua kati ya miaka mitano na saba kuanza kuzaa na mkulima anapata tani 1.6 pekee za mafuta huku za kisasa zinachukua miaka mitatu mpaka mitano kuzaa na mkulima anapata mpaka tani nne za mafuta kwa hekta.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Ezekiel Magehema, alisema wamejipanga kuhakikisha wanawahamasisha wakulima kutumia fursa hiyo kulima zao hilo ili kujiinua kiuchumi.

Alisema tangu mwezi Februari mpaka sasa wataalamu wa kilimo kutoka TARI wamepiga kambi wilayani humo wakitoa elimu na kugawa mbegu za michikichi ili kupanua kilimo hicho.

Alisema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha wananchi kutumia mbegu hizo za kisasa na kuachana na za asili ambazo tija yake ni ndogo ikilinganishwa na za kisasa.