Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 05 03Article 536239

Habari za Biashara of Monday, 3 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TBS yataka wadau wa mchele kuzingatia viwango

Kisukari, saratani tishio vifo hospitalini Kisukari, saratani tishio vifo hospitalini

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele kuzingatia suala la viwango, ubora na usalama wa bidhaa ili kuweza kuongeza tija.

Meneja wa Mafunzo na Utafiti wa TBS, Hamisi Mwanasala, alitoa mwito huo juzi wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk Yusuf Ngenya.

Mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 27, mwaka huu yalifanyika katika wilaya nne kwa nyakati tofauti za Kahama, Bukombe, Katoro, wilayani Geita na kuhitimishwa Sengerema na kunufaisha washiriki zaidi ya 300 katika wilaya hizo.

Katika mafunzo, washiriki walipewa elimu kuhusu TBS na majukumu yake, kanuni bora za uzalishaji, matakwa ya viwango, namna bora ya uhifadhi, ufungashaji na teknolojia ya vifungashio na taarifa za msingi katika vifungashio.

Aidha, alisema washiriki hao walielimishwa juu ya taratibu za usajili wa bidhaa za vyakula, vipodozi na majengo, kazi ambazo hapo awali zilikuwa zikifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Kwa mujibu wa Mwanasala, shirika hilo limeandaa mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kikao kilichofanyika Sirari mkoani Mara, ambacho kiliridhia TBS itoe mafunzo kwa wajasiriamali wanaosindika, kuzalisha, kufungasha na kuuza mchele katika kanda nzima ya Ziwa.

Alisema mafunzo hayo ni uthibitisho wa azma ya serikali kufanikisha malengo ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

"Tuliona mwelekeo mzuri wa usimamizi wa Serikali ambao umeweza kututoa katika uchumi wa chini na sasa tumeingia uchumi wa ngazi ya kati na hata katika awamu ya sita kazi inaendelea," alisema.

Alitoa mwito kwa wanufaika wa mafunzo hayo, kuyatumia watakaporejea kwenye shughuli zao. Aliahidi kuwa TBS itaendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo kwa wazalishaji, wauzaji na wadau wote wa mchele.

Join our Newsletter