Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 08 20Article 552616

Habari za Biashara of Friday, 20 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

TIC, ZIPA kukuza uwekezaji

Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA)

Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) wamekubaliana na kutiwa saini mkataba kwenye ofisi za TIC jijini Dar es Slaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Dk. Maduhu Kazi na Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA, Shariff Ali Shariff kwa lengo la kukuza uwekezaji Tanzania bara na visiwani.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Dk. Kazi alisema miongoni mwa makubaliano hayo ni kutangaza vivutio vya utalii kwa pamoja na kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali.

Dk. Kazi alisema watakuwa wakishirikiana kwa kupeana taarifa mbalimbali za uwekezaji na kushiriki matamasha ya kuhamasisha uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema kwenye makubaliano hayo, pia watashirikiana kufanya utafiti mbalimbali ambao ni muhimu kwa uwekezaji na kubadilishana taarifa, ujuzi na uzoefu kwa masuala ya shughuli hiyo,

“Kuna maeneo ambayo wenzetu ZIPA wako mbele, hivyo tutachota uzoefu wao na sisi kuna maeneo ambayo wanaona tumeenda mbele kuliko wao, hivyo watapenda tuwape siri ya mafanikio ili nao wafikie mafanikio hayo,” alisema.

Dk. Kazi alisema hata kabla ya kutiwa saini kwa ushirikiano huo, kumekuwa na mambo ambayo tayari wameshaanza kushirikiana yakiwamo maonyesho ya kimataifa ya biashara yaliyopita ambapo walikuwa kwenye banda moja.

Alisema kwa mujibu wa mkataba huo, kutakuwa na uwezekano wa kuongeza mambo mengine zaidi ya hayo 12 iwapo wataona kuna haja ya kufanya hivyo na kwamba hilo litawezekana baada ya pande zote kuridhia ongezeko hilo.

“Tutafanyakazi pamoja mfano TIC ikienda kwenye maonyesho ambayo ZIPA haipo basi itawajibika kuelezea vivutio vyake na pia kufanyakazi ya ZIPA kuelezea vivutio vinavyopatikana Zanzibar,” alisema.

Shariff kwa upande wake alisema ushirikiano baina ya taasisi hizo utakuwa na manufaa makubwa kwenye sekta ya uwekezaji kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema kutakuwa na siku ya uwekezaji kila mwaka ambayo itakuwa ikifanyika kwa kupokezana baina ya Tanzania Bara na Visiwani.

Shariff alisema moja ya majukumu yao yatakuwa kuzishauri serikali kuondoa sheria na taratibu ambazo zitaonekana kuwa kikwazo kwa uwekezaji kwa pande zote mbili.