Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 09Article 556294

Habari za Biashara of Thursday, 9 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Taarifa ya NBS kuhusu hali ya uchumi nchini Tanzania

Taarifa ya NBS kuhusu hali ya uchumi nchini Tanzania Taarifa ya NBS kuhusu hali ya uchumi nchini Tanzania

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza kuwa mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi kati ya Januari-Juni mwaka huu vinaonesha uchumi wa nchi unaendelea kuimarika.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Daniel Masolwa jijini Dodoma September 8, 2021.

Masolwa amesema viashiria hivyo vipo katika maeneo manne likiwemo la kuongezeka kwa idadi ya watalii, uzalishaji wa saruji, huduma za mawasiliano na uzalishaji wa nishati ya umeme.

Amesema hayo wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa Agosti ambao umebaki asilimia 3.8 kama ulivyokuwa Julai mwaka huu.

Kuhusu kiashiria cha idadi ya watalii, katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, alisema:”Idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini katika kipindi hicho walitoka Urusi. Mwenendo huo unaashiria kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini.”

Kuhusu kiashiria cha uzalishaji wa saruji alisema umeendelea kuimarika. Kuhusu huduma za mawasiliano alisema ongezeko la huduma hizo limetoka dakika za kuzungumza bilioni 31.3 katika kipindi cha Januari -Juni 2019 hadi dakika bilioni 42.9 katika kipindi kama hicho mwaka huu.

Amesema mwenendo wa uzalishaji wa nishati ya umeme umendelea kuwa imara ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka saa za kilowati milioni 3,478 katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018 hadi saa za kilowati milioni 4,053 katika kipindi hicho mwaka 2021.

Mkurugenzi wa Sensa za Takwimu za Jamii, Ruth Minja amesema mfumuko wa bei kwa Agosti umebaki kwa asilimia 3.8 kama ilivyokuwa Julai mwaka huu.

“Hiyo ina maanisha kwamba kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa Agosti mwaka huu imekuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa Julai mwaka huu,” alisema Minja.

Amesema mfumo haukuongezeka kwa sababu kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula. Bidhaa zilizopungua bei ni nafaka yakiwemo mahindi na unga wa mahindi kwa asilimia 4.7, nyama asilimia 6.3, mboga 2.3, maharage 4.7.

Bidhaa zisizo za vyakula zilizoongeza bei ni mavazi asilimia 4.7, mkaa 1.9, gesi 2.1, kodi ya pango 5.1 na gharama za malazi kwa wageni asilimia 5.3.

Mchumi Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Stanislaus Thadeus alisema mfumo wa bei wa chini uliotulia unachangia kuwepo kwa maendeleo na ustawi wa jamii na hivyo kuongeza uwezo wa kukua uchumi na jamii kustawi.