Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 04Article 540979

xxxxxxxxxxx of Friday, 4 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanesco yakusanya bil 160/- kwa mwezi

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia wastani wa Sh bilioni 160 kwa mwezi.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, alibainisha hayo bungeni wakati akieleza mafanikio ya sekta ya nishati alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema mapato ya Tanesco yameongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 72 kwa mwezi mwaka 2016 hadi kufikia wastani wa Sh bilioni 160 kwa mwezi mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la takriban asilimia 102.

"Ongezeko hili pia limetokana na kutumia mfumo wa LUKU (Lipia Umeme Kadiri Unavyotumia) wa kulipa ankara za umeme kwa wateja wote nchini," alisema Kalemani.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuongeza kasi ya kufuatilia madeni sugu ya wateja wa Tanesco na kupungua kwa madeni kutoka Sh bilioni 272 mwaka 2017 kufikia Sh bilioni 48.9 mwaka 2020.

Mafanikio mengine ni Tanesco kuendelea kujitegemea na kuendesha shughuli bila kupata ruzuku ya takriban Sh bilioni 143 kwa mwaka kutoka serikalini.

Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali kupitia Tanesco na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeendelea kuunganisha umeme kwa Sh 27,000 katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na mitaa katika majiji na manispaa kulingana na mpango wa kupeleka umeme vijijini.

"Pia kuongeza matumizi ya nguzo za zege katika kujenga njia za kusafirisha umeme katika baadhi ya maeneo yenye mahitaji hayo.”

“Aidha, viwanda vya ndani vya kuzalisha nguzo za zege vimeongezeka kutoka kimoja mwaka 2018 na kufikia vitano vinavyozalisha zaidi ya nguzo 15,000 kwa mwaka," alisema Kalemani.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuondoa hasara ya Tanesco zilizokuwepo za Sh bilioni 349 katika kipindi cha miaka 2015-2017.

"Hasara hizi, pamoja na mambo mengine zilizotokana na kutumia mafuta mazito na kuagiza vifaa kutoka nje ya nchi," alisema.

Alisema mengine ni kuondoa gharama kubwa wanazotozwa wananchi wa kawaida za kuuziwa umeme na wazalishaji wadogo kutoka Sh 3,500 au zaidi kwa uniti moja ya umeme hadi Sh 100 kwa uniti kama inavyotozwa na Tanesco.

Akitaka mafaniko mengine, Dk Kalemani alisema ni pamoja na kuendelea na Ujenzi wa Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power Project ambao umefikia asilimia 52, na Mradi wa Rusumo MW 80 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 80.

Mengine ni kuanza maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya kufua umeme ya Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222).

Alitaja pia kukamilika kwa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme msongo wa kV 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita yenye urefu wa kilomita 55 uliokamilika mwezi Septemba, 2020 na kuunganisha umeme vijiji takriban 10 katika Wilaya ya Geita vinavyopitiwa na mradi huo.

Mengine ni kukamilika kwa ujenzi wa Mradi wa Njia ya Kuendesha Treni ya Kisasa ya Mwendokasi ya kutumia umeme.

Awamu ya Kwanza yenye urefu wa kilomita 160 kutoka Dar es Salaam hadi Kingolwira, Morogoro ilikamilika mwezi Septemba, 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 76.26 kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.

"Kukamilika kwa mradi huu kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuanza kuendesha treni ya kisasa ya mwendokasi ya kutumia umeme katika nchi za Afrika Mashariki," alisema.

Alisema pia kuendelea na Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2021 jumla ya vijiji 10,312 vimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa vimeunganishwa umeme mwaka 2015 sawa na ongezeko la vijiji 8,294 sawa na asilimia 86 ya vijiji vya Tanzania Bara vimepata umeme.

Alisema pia kuendelea kuhamasisha na kusisitiza uzalishaji wa vifaa vya kujenga miradi ya umeme nchini na kuzuia uingizaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo, mashineumba (transfoma), nyaya na mita za LUKU ndani ya nchi na hivyo kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo na kuokoa takriban Sh bilioni 162.23.

Kalemani alisema: "Uzalishaji huo pia umechangia ongezeko la ajira nchini ambapo Watanzania wapatao 22,820 wameajiriwa katika viwanda hivyo kati ya mwaka 2017 hadi sasa."

Pia kuendelea kuunganisha umeme wateja wapya nchini kwa kasi ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Machi, 2021 Watanzania wanaonufaika na huduma ya umeme wamefikia takriban milioni 47 sawa na asilimia 78 ya Watanzania wapatao milioni 60.

Join our Newsletter