Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 08Article 562129

Habari za Biashara of Friday, 8 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania kuongeza ndege 5 zaidi

Tanzania kuongeza ndege 5 zaidi Tanzania kuongeza ndege 5 zaidi

SERIKALI imepokea ndege mbili huku ikiweka lengo la kufikia ndege 16 ifikapo mwaka 2023.

Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, katika mapokezi ya ndege mbili aina ya Airbus A220 – 330 Tanzanite na Zanzibar.

Amesema mipango inaendelea ya kufikisha idadi hiyo ya ndege 16 ambapo mpaka sasa ndege ambazo tayari zimefika nchini kuwa 11.

Ndege nane ambazo tayari zimepokelewa nchini ni ndege aina ya Bombardier Dash 8 Q-400, ndege aina ya Boeing 787 – 800 Dreamliner, Airbus A220-300.

Rais Mwinyi alisema sababu kuu zilizochochea serikali kufufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa, ilikuwa aibu kutokuwa na ndege hivyo mkakati wa serikali ni kuongeza ndege tano zaidi na kufikia ndege 16 ifikapo 2023.

Alisema pia ni kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kuyafikia masoko ya kimataifa kwa urahisi na kukuza sekta ya utalii ambapo licha ya Tanzania kuwa ya pili kwa vivutio vingi vya utalii duniani, bado idadi ya watalii wanaoitembelea sio wengi kutokana na uwezo mdogo wa kusafirisha watalii kwa kuwa bado inategemea ndege za nje kuleta watalii.

Aidha alisema sekta ya usafirishaji wa anga, majini na nchi kavu, ni msingi muhimu wa uchumi wa taifa na mataifa yote duniani.

“Sekta ya usafirishaji ndio msingi mkubwa katika kukuza sekta za utalii, biashara, kilimo, viwanda, madini pamoja na kurahisisha shughuli za watu,” alisema

Alisema vile vile maendeleo katika usafiri wa anga yana uhusiano na ukuaji wa ajira sio tu katika viwanja vya ndege hata sekta nyingine.

“Serikali zote mbili kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imedhamiria kwa dhati mwaka 2025 kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa kujenga na kuimarisha miundo mbinu ya kisasa ya barabara, bandari na ndege.

“Mkataba wa kimataifa wa kiwanja cha ndege cha Msalato umesaini Septemba 13, serikali ya Zanzibar pia ipo kwenye mazungumzo na wawekezaji kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Pemba.”alisema