Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 08 13Article 551284

Habari za Biashara of Friday, 13 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Metacha anahitaji zaidi msaada wa kisaikolojia

UCHAMBUZI: Metacha anahitaji zaidi msaada wa kisaikolojia UCHAMBUZI: Metacha anahitaji zaidi msaada wa kisaikolojia

YANGA wamewaacha baadhi ya wachezaji wao ambao mikataba yao imemalizika akiwamo kipa Metacha Mnata. Huyu alisimamishwa kabla hata Ligi Kuu Bara haijamalizika kutokana na utovu wa nidhamu.

Metacha alionyesha ishara ya matusi baada ya mashabiki kumshutumu kufungwa bao la kizembe katika mechi waliyoshinda 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting Juni 17, 2021, kitendo kilichoifanya Bodi ya Ligi (TPLB) kumfungia mechi tatu na kumtoza faini ya Sh.500,000.

Kabla ya Bodi ya Ligi kumfungia, Uongozi wa Yanga ulishachukua hatua ya kinidhamu kwa kipa huyo wakimsimamisha kwa muda usiojulikana hadi hivi karibuni walipotangaza kuachana naye.

Ikumbukwe kwamba tuhuma ama malalamiko kwa Metacha hayakuanzia katika mechi hiyo pekee bali hali hapo awali alilalamikiwa ingawa wengine walimtetea kuwa huenda hayupo sawa kiakili kutokana na matatizo aliyokuwa ameyapata ya kuondokewa na mwanaye.

Yote yanawezekana kwani binadamu yeyote ni lazima ataumia anapoondokewa na mwanaye ama ndugu wa karibu na pengine hata uwezo wa kufikiri pia hushuka kwa kiasi fulani kutokana na msongo wa mawazo. Hicho huenda kilitokea hata kwa kipa huyo.

Wakati hayo yote yanatokea pengine Metacha hakupata washauri wa kisaikolojia kwa haraka hivyo alijikuta kana kwamba lolote analolifanya lipo sawa kwa wakati huo na linapotokea majuto humpata baadaye lakini huku tayari akiwa amefanya jambo la kuwakera mashabiki wake.

Kipa huyo bado ni kijana mdogo kiumri na huenda anayoyapitia ni makubwa kuliko umri wake ingawa kuna wengine wenye umri kama huo wana uwezo wa kuyabeba mapito yao na hiyo hutegemea na nani yupo nyuma yao.

Sidhani kama hivi sasa Metacha anaweza kuzichezea tena timu kubwa kama Simba ama Azam FC kwani huko tayari nafasi zimejaa na hata kama hazijajaa tabia za hizi timu ni mara chache zikachukuwa mchezaji ambaye ameachwa kwa utovu wa nidhamu hasa tena kwa nafasi kama yake.

Hata hivyo, kabla ya kipa huyo kuanza mchakato wa kusaka timu nyingine kwa msimu ujao ni lazima wanaomsimamia wafanye jambo la kumsaidia kipa huyo ili asipotee zaidi yaani atakakokwenda aende na akili mpya na kutojutia uamuzi ya kuachwa kwenye timu kubwa.

Naamini bado ana nafasi nyingine ya kucheza kwa nidhamu kubwa kwani uwezo huo anao, lakini angalizo tu kwa wale wanaosimamia wachezaji kuwa karibu na wachezaji wao hata pale wanapopata matatizo ili yasiwaondoe kwenye viwango vyao, wasisubiri tu wakati wa kusaini ndipo wapiganie maslahi yao kwasababu tu watapata 10%.

Kuwasaidia wakati wa kusaini mikataba pekee, huo si msaada kwa wachezaji bali ni kuwageuza mgodi wa kuchimba madini tu kujinufaisha. Hata kama Metacha alikuwa na matatizo mengine ya kisoka huko nyuma lakini yasingemfikisha hapa alipo sasa na kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Naamini Metacha ana wasimamizi kwenye soka lake. Hao wasimamizi kama watashindwa wao kumjenga kisaikolojia basi wamtafutie mtaalamu wa saikolojia ili amwandae kabla hajaenda kwenye timu nyingine ambako anapaswa kwenda na akili mpya na ya ushindani vinginevyo anaweza pia kujiona si lolote kwenye mpira huu na kupotea kabisa.

Kwa muonekano wa nje, Metacha anategemea maisha yake kuendesha kupitia soka, sijui kwa ndani kama ana shughuli nyingine ama kazi inayomwingizia kipato. Hivyo ni lazima kuhakikisha akili yake inakaa sawa muda wote.

Nimeyazungumza yote hayo kwasababu hata alipopewa barua ya kuachwa alifuta picha zote kwenye mitandao yake ya kijamii alizopiga akiwa amevaa jezi za Yanga, hiyo tu inaonyesha kuwa hayupo sawa kuna jambo linamkwaza na kumuumiza.

Hajaona thamani yoyote ya kuwepo ndani ya Yanga kwa kipindi chote alichoitumikia klabu hiyo sio kama wenzake ambao hushukuru hata kama wamepitia changamoto pengine kubwa kuliko hata zake.

Yawezekana ni jambo la kawaida tu kufuta hizo picha lakini kwa mtu muungwana na mwenye kutambua thamani hata ile kidogo tu ya kule alikotoka hawezi kufanya hivyo bali wengi wafanyayo hivyo mara nyingi hufanya wakiwa na hasira ndio maana naelezea kwa kipa huyo anapaswa kujengwa zaidi kiakili kwani anaishi na hasira akilini mwake jambo ambalo si zuri kiafya.