Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 14Article 563173

Habari za Biashara of Thursday, 14 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ukuaji uchumi nchini waongezeka asilimia 0.3

Ukuaji uchumi nchini waongezeka asilimia 0.3 Ukuaji uchumi nchini waongezeka asilimia 0.3

UKUAJI wa uchumi katika robo ya pili ya mwaka 2021 (Aprili –Juni) umefi kia asilimia 4.3 kutoka asilimia 4.0 ya kipindi kama hicho mwaka jana. Ukuaji huo unakadiriwa hadi mwisho wa mwaka huu utaongezeka hadi asilimia tano.

Ongezeko hilo la ukuaji wa uchumi ni sawa na asilimia 0.3 ukilinganisha na robo ya pili ya mwaka jana. Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi NBS, Daniel Masolwa alisema jana Dodoma kuwa katika kipindi cha robo ya pili katika mwaka jana, uchumi uliongezeka kwa kasi ndogo ya asilimia 4.0 iliyosababishwa na athari za ugonjwa wa Covid-19.

“Sekta ya utalii imeendelea kuimarika zaidi kufuatia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini.” Masolwa alisema kasi ya ukuaji wa pato la taifa kwa robo mwaka kati ya mwaka 2017 na 2021, unaonesha kwamba mwaka 2017 kasi ya ukuaji ni kwa wastani wa asilimia 6.7, ambapo katika robo ya kwanza pato lilikua kwa asilimia 4.9, ya pili 6.7, ya tatu 5.0 na ya nne 10.2.

Mwaka 2018, kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa lilikuwa ni kwa wastani wa asilimia 7.0 ambapo robo ya kwanza lilikua kwa asilimia 7.5, ya pili 6.0, ya tatu 7.2 na ya nne 7.1.

Mwaka 2019 kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 7.0 ambapo robo ya kwanza lilikua kwa asilimia 6.2, ya pili 7.4, ya tatu 8.1 na ya nne 6.4. Mwaka 2020 kasi ya ukuaji wa pato la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 4.8 ambapo robo ya kwanza kwa asilimia 5.9, ya pili 4.0, ya tatu 4.4 na ya nne 4.8.

Mwaka huu katika robo ya kwanza pato lilikua kwa asilimia 5.0 na robo hii ya pili kwa asilimia 4.3. Hata hivyo, Pato la Taifa kwa bei kwa miaka husika (2017-2021) liliongezeka hadi Sh trilioni 39.2 kutoka Sh trilioni 37.2 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2020. Lakini pia, Pato Halisi la Taifa katika mwaka 2021 liliongezeka hadi Sh trilioni 33.4 kutoka Sh trilioni 32.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Katika kipindi cha robo ya pili (Aprili-Juni) ya mwaka 2021, shughuli za habari na mawasiliano ziliongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa asilimia 12.3, zikifuatiwa na shughuli za uzalishaji umeme (12.3).

Shughuli nyingine zilizokuwa na kiwango cha juu na asilimia kwenye mabano ni huduma za jamii zikijumuisha sanaa na burudani na shughuli za kaya katika kuajiri |(10.8), malazi na huduma za chakula (10.1), usambazaji maji (8.4) na uchimbaji wa madini na mawe (7.3).

Masolwa alisema mchango wa shughuli kuu za kiuchumi katika Pato la Taifa kwa kiwango kikubwa huduma zilichangia kwa asilimia 38.9, zikifuatiwa na shughuli za msingi kwa asilimia 36.9 na shughuli za kati 24.2. Katika robo ya pili ya mwaka huu, ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.3 ulichangiwa na shughuli zote za uchumi, lakini sekta zilizotoa mchango mkubwa ni kilimo kwa asilimia 13.0, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (8.4), biashara na matengenezo (8.1), viwanda (7.6), madini (7.6) na ujenzi (7.1).