Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 24Article 544069

Habari za Biashara of Thursday, 24 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Uzalishaji chai kuongezwa hadi tani mil. 60

Kilimo cha Chai Kilimo cha Chai

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda, aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akizindua programu ya kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya kahawa, chai, mboga na matunda ijulikanayo ‘Agri-Connect’ inayotarajiwa kutekelezwa katika mikoa sita ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar.

Programu hiyo ambayo inafadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) kwa Dola za Kimarekani milioni 100 (Sh. bilioni 273), inatarajiwa kutekelezwa kwa miaka minne.

Prof. Mkenda alisema watafiti wamebainisha kwamba Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa uzalishaji wa chai kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, lakini uzalishaji bado upo chini.

Alisema katika Kitabu cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, imeelezwa mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ili kuliwezesha taifa kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya mazao hayo.

“Sasa hii programu nitaifuatilia mimi mwenyewe ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya na sitegemei hizi fedha zitumike kwa ajili ya vikao na kulipana posho, itatusaidia sana kufikia malengo yetu ya kuongeza uzalishaji wa chai na mazao mengine,” alisema Prof. Mkenda.

Alisema katika nchi za Afrika Mashariki, Kenya ndiyo inayoongoza kwa kuzalisha chai nyingi, kwa mwaka wanazalisha tani milioni 500 na kuna uwezekano Tanzania ikawa inazalisha zaidi kuliko nchi hiyo.

Alisema yapo mashamba katika mikoa ya Iringa na Njombe, ambayo yalikuwa yanalimwa, lakini yalitelekezwa na serikali inakusudia kuyafufua na kufungua mapya kwenye maeneo mengine.

Balozi wa EU nchini, Manfredo Fant, alisema mbali na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao hayo, pia programu hiyo ina malengo mengine ikiwamo kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini ili kuwawezesha wakulima kuyafikia masoko kiurahisi.

Alisema baadhi ya barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami na zingine kwa kiwango cha changarawe na kusaidia kwenye uboreshaji wa sera za nchi hasa kuhusu biashara za mazao.

Vilevile, alisema programu hiyo inalenga kuboresha lishe kwa wananchi ili kukabiliana na tatizo la udumavu linalowatesa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

“Tukiboresha miundombinu ya barabara tutakuwa tumewasaidia wakulima kuepuka asilimia 46 ya upotevu wa mazao ambayo wanapoteza sasa hivi, na itasaidia kuinua uchumi wao,” alisema Balozi Fant.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Christina Ishengoma, aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa ufadhili wa programu hiyo kuwa ina faida kubwa kwa taifa.

Alisema programu hiyo itasaidia kupunguza tatizo la udumavu ambalo limekuwa sugu nchini huku akiwataka viongozi wa maeneo yote ambayo programu hiyo itatekelezwa kutoa ushirikiano ili ifanikiwe.

Mikoa sita ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayotarajiwa kunufaika na programu hiyo ni Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe na Katavi na zaidi ya wakulima 220,000 wanatarajiwa kunufaika.