Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 05Article 561358

Habari za Biashara of Tuesday, 5 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Vituo 25 kutoa huduma ya gesi kwenye magari

Vituo 25 kutoa huduma  ya gesi kwenye magari Vituo 25 kutoa huduma ya gesi kwenye magari

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limejiwekea malengo vituo 25 vya mafuta viwe vinatoa huduma ya nishati ya gesi kwenye magari ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha 2021/2022.

Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi aliyasema hayo jana kupitia salamu zake katika maadhimisha ya Siku ya Makazi Duniani.

Alisema TPDC imefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha katika usimamizi wa usambazaji wa gesi asili kwa matumizi ya kupikia majumbani, hotelini na katika taasisi za umma nchini.

Alisema shirika hilo limeanza kuhamasisha wamiliki na watumiaji wa vyombo vya moto ili vitumie nishati ya gesi asili inayozalishwa kwa wingi nchini.

“Katika kufanikisha matumizi ya gesi asili kama mbadala wa mafuta ya petroli, TPDC inawahimiza wamiliki wa vituo vya mafuta nchini kuanza kutoa huduma ya mauzo ya gesi asilia katika vituo vyao kwa ajili ya matumizi ya magari,” alisema Lukuvi.

Alisema Siku ya Makazi Duniani hutoa fursa kwa kila taifa, wananchi na wadau wengine wa makazi kutafakari kila mmoja kwa nafasi yake namna alivyoshiriki na atakavyoshiriki kuboresha makazi hasa katika miji na majiji.

“Kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa jamii ya kimataifa inalazimika kujiandaa vyema kuishi maisha ya kimji. Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu ‘Utekelezaji wa haraka wa majukumu ya kimji ili kuwa na dunia isiyo na hewa ukaa.’

Lukuvi alisema hewa ukaa au kaboni ni hewa chafu inayozalishwa kila siku duniani kutokana na shughuli za kiuchumi na za kijamii na kwamba imesababisha utando mzito katika anga la juu linaloizunguka dunia na hivyo kusababisha mabadiliko hasi ya tabianchi.

Alitaja matokeo hasi ya mabadiliko ya tabianchi kwa miongo kadhaa sasa ni ongezeko kubwa la joto, vimbunga vikali, mafuriko kutokana na mvua kubwa zisizo za kawaida, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari na milipuko ya maradhi.

Alisema kuchafuka kwa anga la juu la dunia kunachochewa kwa kiwango kikubwa na mataifa yaliyoendelea kutokana na matumizi makubwa ya nishati ya mafuta na mataifa hayo makubwa kiuchumi kuwa chanzo kikubwa cha uzalishaji wa hewa ukaa duniani.

“Ukweli ni kwamba, kila nchi na kila mwananchi anahusika kwa namna moja au nyingine katika uzalishaji wa hewa ukaa duniani. Mfano, matumizi ya kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia majumbani, matukio ya uchomaji hovyo wa mashamba na misitu, uchomaji wa taka ngumu majumbani, pamoja na uvunaji usioendelevu wa rasilimali misitu ni vyanzo dhahiri vinavyozalisha hewaukaa duniani,” alisema.

Lukuvu alisema takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) zinaonesha kuwa, miji na majiji kote duniani yanatumia zaidi ya asilimia 75 ya nishati na kuzalisha takriban asilimia 70 ya hewa ukaa duniani.

Alisema katika kuadhimisha siku hiyo ni vyema kila mwananchi atambue kuwa serikali imefanya juhudi kubwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa hususani kwa wakazi wa mijini na kutolea mfano, usambazaji wa nishati ya umeme kwa gharama nafuu mijini na vijijini, uhamasishaji wa matumizi ya gesi ya kupikia majumbani na upigaji marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

Alisema wizara yake kupitia watalaamu imetoa mchango mkubwa katika kupunguza ongezeko la hewa ukaa katika miji na majiji kwa kupanga miji, kutunza vijito asili, maeneo oevu, mabonde na miinuko pamoja na kuhifadhi misitu ya asili.