Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 04 07Article 532288

Business News of Wednesday, 7 April 2021

Chanzo: HabariLeo

Viwanda, Kilimo watakiwa kusaka masoko

Viwanda, Kilimo watakiwa kusaka masoko

WIZARA ya Viwanda na Biashara kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo zimetakiwa kubuni utaratibu utakaowezesha wakulima wa Tanzania kupata masoko ya mazao yao nje ya nchi bila usumbufu wowote.

Rai hiyo imetolewa jana na Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake kwa taifa wakati alipowaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za umma Ikulu, Dar es Salaam.

Alisema ingawa Watanzania wanajitahidi kuzalisha mazao mbalimbali, lakini hali ya masoko sio rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kwa sababu hakuna utaratibu wa kujua mazao yanayotarajiwa kuzalishwa nchini.

Alisema ni lazima wizara hizo kuweka utaratibu wakujua idadi ya tani zinazozalishwa na kujua kiwango cha mazao yatakayotumika kama chakula cha ndani na pia kiwango kitakachouzwa nje ili kuweka utaratibu wa namna mazao hayo yatakavyouzwa nje.

“Je soko la nje ni lipi na wapi? Mmeongea nao vipi, makubaliano mliyofikia nao ni yapi? Halafu baada ya hapo mnawaachia wakulima wauze vitu vyao,” alisema Rais Samia.

Alisema utaratibu wa sasa wa kuwaachia wakulima peke yao wavune waweke mazao yao ndani soko hakuna wakipeleka nchi jirani wanazuiwa.

“Halafu na wizara mpo tu hamjali wakulima wanapata shida gani mmeng'ang'ania tu wizara ya viwanda, biashara na masoko, hayo masoko yako wapi?” alihoji Rais Samia.

Kiongozi huyo wa nchi aliwaagiza viongozi wa wizara hozo kwenda kujipanga upya na kuangalia utaratibu utakaowezesha Tanzania kupata masoko ya kutosha nje ya nchi.

Join our Newsletter