Uko hapa: NyumbaniBiashara2022 01 13Article 585418

Habari za Biashara of Thursday, 13 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Wachimbaji Tanzanite watakiwa kufufua migodi 1,700

Wachimbaji Tanzanite watakiwa kufufua migodi 1,700 Wachimbaji Tanzanite watakiwa kufufua migodi 1,700

Wamiliki wanaochimba migodi ya madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wametakiwa kulipia leseni wanazozimiliki ili waendelee kufanya kazi.

Zaidi ya migodi 2,000 ya madini ya Tanzanite imekatiwa leseni ya uchimbaji ila iliyopo hai na inayofanyiwa kazi ni migodi 300 pekee.

Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Fabian Mshai ameyasema hayo wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani.

Mshai amesema wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite wanaodaiwa fedha za leseni wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kulipa ili kuondokana na kufuatanafuata.

Amesema leseni zisipofanyiwa kazi zinasababisha madeni kwani wanapoomba wanapaswa kuziendeleza kwa kuhakikisha zinafanya kazi.

"Hivi sasa kuna madeni mengi ya fedha za leseni takribani Sh300 milioni hivyo wale wote wanaodaiwa wafike ofisini ili walipe na kuendeleza sekta," amesema Mshai.

Katibu wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoa wa Manyara (Marema), Tariq Kibwe amesema suala la wachimbaji kulipia leseni zao halikwepeki hivyo watekeleze suala hilo.

Ofisa mkaguzi wa migodi, mhandisi Castro Maduwa amesema wachimbaji wanaponunua zana za milipuko wanapaswa kuwa na vibali ili kuepusha ajali zisizokiwa za lazima. Mwenyekiti wa Tanzanite, Money Yusuf amesema mchimbaji anapaswa kuzingatia agizo la kuwa na kibali cha milipuko kwani wanaweza kukamatwa na Serikali.