Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 12Article 542311

Habari za Biashara of Saturday, 12 June 2021

Chanzo: millardayo.com

"Wafanyabiashara wadogo wanahitaji kukua" - NBC

Benki ya Taifa ya Biashara leo imezindua kampeni yake ya Twende Sawa na NBC yenye lengo la kuwafuata na kuwapa elimu wafanyabiashara wanaochipukia katika maeneo yao ya kazi na biashara. Kampeni hiyo imezinduliwa leo katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbali mbali wakiwemo wafanyakazi na baadhi ya wateja wa benki hiyo.

Lengo kubwa la kampeni ya Twende Sawa na NBC ni kutoa elimu ya kuendesha biashara, usimamizi makini wa wapato, urasimishaji wa biashara pamoja na kuweka kumbukumbu za kifedha ili kumuwezesha mfanyabiashara anayechipukia kusimamia na kuendesha baishara yake kwa ufanisi zaidi. Pamoja na elimu itakayotolewa, kampeni ya Twende Sawa na NBC pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara kufungua Akaunti ya Kua Nasi yenye masharti nafuu kufungua, inayotoa riba kwa amana za mteja pamoja na kutokuwa na gharama za uendeshaji za kila mwezi.

Akiongea katika hafla hiyo ya uzinduzi, Mkurugenzi wa Wateja wa Rejareja na Binafsi wa NBC, Nd Elibariki Masuke alisema kuwa lengo kubwa la Benki ya Taifa ya Biashara ni kuwa karibu zaidi na wafanyabiashara wadogo ili wawawezeshe kukuza biashara sambamba na benki hiyo. Aidha alisema kuna maboresho ambayo benki hiyo imekuwa ikifanya ili kutimiza lengo la kuwa karibu zaidi na wafanyabiashara wadogo.

“Tumeongeza wigo wa matawi ya benki yetu nchini kupitia NBC Wakala na tumeweka mfumo wa kidijitali wa kufungua akaunti, tumerahisisha ufunguaji wa akaunti ambapo mtu anahitaji kitambulisho chake cha NIDA tu hivyo tumejipanga kuwaifikia na kuwahudumia kikamilifu wafanyabisahara wa jiji la Dar es Salaam na na maeneno mengine ya nchi kote.” Masuke.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya NBC, Nd Raymond Urassa ambaye ndiyo msimamizi wa Akaunti ya Kua Nasi amasema akaunti hiyo ni mahususi na ni rafiki kwa wafanyabiashara wadogo.

“Sisi kama NBC tunatambua kwamba wafanyabiashara wadogo wanahitaji kukua kupitia benki yetu ndiyo maana tumeondoa makato ya uendeshaji ya kila mwezi, tunampa mjasiriamali faida kwa hela atakayokuwa ameweka, tunatoa vitabu vya hundi kwa gharama nafuu watakaohitaji lakini pia tumepunguza gharama za utoaji wa fedha kupitia akaunti hii ya Kua Nasi ili kumpa mjasiriamali fursa ya kukua zaidi.” Raymond

Akielezea akaunti hiyo, Raymond Urassa alisema kwamba mfanyabiashara yeyote mdogo anaweza kufungua Akaunti ya Kua Nasi kupitia matawi yote ya Benki ya Taifa ya Biashara nchi nzima lakini pia kupitia mawakala wa benki hiyo ambao pia wanapatikana nchi nzima.