Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 22Article 573439

Habari za Biashara of Monday, 22 November 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wafanyabiashara waitaka ofisi ya TRA kujenfa soko la madini

Wataka ofisi ya TRA soko la madini Wataka ofisi ya TRA soko la madini

WAFANYABIASHARA wa madini ya dhahabu katika soko la madini wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufungua ofisi katika soko hilo ili kupata urahisi wa ukaguzi wa nyaraka zao.

Ukaguzi huo ni wa kabla ya usafirishaji wa madini kwenda katika masoko ya kitaifa.   Walidai kuwa, ofisi ya TRA iliyopo ipo katika Mji Mdogo wa Isaka katika Halmashauri ya Msalala, ambapo inachukua umbali wa kilometa 40 kutoka mjini Kahama kufika, kitu ambacho kimekuwa kikisababisha kuachwa na ndege wakati wa usafirishaji wa madini hayo.   Hayo yalibainishwa na Meneja wa Kampuni ya Sub Gold Limited (SGL), Abdulrahim Sangey, wakati akizungumza na vyombo vya habari, na kueleza changamoto ambazo wanakutana nazo wakati wa usafirishaji wa madini kwenda katika masoko ya kimataifa nchi za nje.   Sangey alisema, kutokana na wakaguzi wa mamlaka hiyo kuwa Isaka, wanalazimika kuchelewa usafiri wa ndege zinazokuwa zinatua katika uwanja wa Buzwagi mara mbili kwa wiki, hivyo kusafiri hadi jijini Mwanza kwa njia ya barabara, jambo ambalo ni hatari kupoteza mzigo na linawagharimu fedha nyingi na kuhatarisha usalama wa mali zao.   Naye Emmanuel Sadick, alisema kuna wakati wanasafirisha mzigo nyakati za usiku kwenda jijini Mwanza  kwa ajili ya kuwahi ndege zinazokuja kuchukua madini hayo baada ya kuchelewa kupata nyaraka za TRA, jambo ambalo lilikuwa linawezekana kutatuliwa endapo ofisa wa mamlaka hiyo angekuwa ndani ya soko la madini au katika ofisi kuu iliyopo Manispaa ya Kahama.   Meneja wa TRA mkoa wa kikodi wa Kahama, Warioba Kanire, alisema atalifuatia tatizo hilo kwa ukaribu kuangalia namna ya kulitatua ili kuongeza msukumo wa ufanyaji kazi na kuondoa malalamiko ambayo yameanza kuibuka.   Aidha, alisema kwa anavyofahamu, baada ya wafanyabiashara wa madini kumaliza kufunga mali zao kwa ajili ya usafirishaji, maofisa kutoka ofisini kwake wamekuwa wakifika katika soko la madini kukagua nyaraka mbalimbali za usafirishaji wa madini hayo.   Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, alifanya ziara katika soko kuu la madini ya dhahabu Manispaa ya Kahama, kwa lengo la kuangalia shughuli ambazo zinaendelea na kuzungumza na wafanyabiashara waliopo na kusikiliza changamoto ambazo zinawakabili.