Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 10Article 556606

Habari za Biashara of Friday, 10 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wafanyabiashara watajwa kuwa kikwazo mfumo wa Stakabadhi Ghalani

Wafanyabiashara watajwa kuwa kikwazo mfumo wa Stakabadhi Ghalani Wafanyabiashara watajwa kuwa kikwazo mfumo wa Stakabadhi Ghalani

WAFANYABIASHARA na wadau wanaonufaika na mifumo isiyo rasmi kwenye ununuzi wa mazao, wamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala, imebainika.

Hayo yamebainishwa jijini hapa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Msimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu (pichani), wakati wa kuelezea utekelezaji wa mfumo huo.

Alisema moja ya changamoto zinazokabili utekelezaji wa mfumo huo ni pamoja na upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara na wadau wengine wanaonufaika na mifumo isiyo rasmi sambamba na uelewa mdogo wa mfumo huo.

Alisema kumekuwa pia na maagizo pinzani na Sheria ya Stakabadhi za Ghala wakati wa utekelezaji wa mfumo huo kama vile zuio la kuendelea na shughuli kwa baadhi ya mikoa na uhaba wa maghala bora.

Alisema changamoto nyingine ni wadau saidizi kama vile vyama vikuu kuchelewesha malipo kwa wakulima, licha ya fedha kulipwa kwa wakati katika akaunti zao, hali inayofanya wadau kuona kama mfumo unaleta usumbufu kwa wakulima.

“Pia kutoanza kutumika kwa soko la bidhaa katika baadhi ya mazao kama vile kokoa na kusuasua kwenye korosho licha ya sheria na taasisi kuwa tayari zimeundwa,” alisema.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa fedha na vitendea kazi kwa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala unaosababisha kazi za Bodi kufanywa katika mazingira magumu.

Kuhusu fursa za mfumo wa stakabadhi za ghalani endapo utatekelezwa katika mazao na bidhaa nyingine kama vile mkonge, pamba, nafaka, bidhaa za mifugo na misitu, pato la mkulima na la taifa litaongezeka kama ilivyo kwa mazao ya ufuta na choroko yaliyomo kwenye mfumo huo.

Aidha, Bangu alisema kwa sasa mtazamo wa bodi ni kwamba mfumo huo ukitekelezwa katika bidhaa mbalimbali zikijumuisha bidhaa za kilimo na bidhaa zisizo za kilimo, utaleta manufaa makubwa kwa wazalishaji wa bidhaa kwa wakulima, wafugaji na wasindikaji.

“Pia mfumo utaongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani kwenye masoko ya nje na kuongeza uzalishaji wa mazao, upatikanaji wa takwimu sahihi za bidhaa zinazozalishwa na kuongeza mapato katika halmashauri na Serikali Kuu,” alisema.