Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 10Article 542050

Habari za Biashara of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wakulima wa parachichi wajitengeneza kukopa TADB

WAKULIMA wadogo wa zao la parachini wilayani Songea mkoani Ruvuma, wamewaalika maofisa wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kujionea hali halisi ili kuwapa mikopo ya kuwawezesha kulima zao hilo kibiashara na kwa tija zaidi.

Hao ni wakulima wa parachichi waliotikia mwito wa kulima kisasa zao hilo kama zao la biashara.

Akizungumza baada ya mkutano wa tathimini ya kilimo hicho kipya mkoani humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lusitu Agro-Business, Beno Mgaya alisema vikundi vyote saba vilivyofanya mikutano ya tathimini, vimeazimia kualika watendaji wa TADB kwenda mkoani humo kujionea mahitaji ya mtaji katika kuandaa mashamba ya maparachi ili kilimo chao kiwe cha kisasa.

“Katika vikundi saba ambavyo vimefanya mapitio ya juhudi zao, imekuwa wazi kwamba mtaji thabiti unahitajika kuandaa ekari moja ili kilimo kiwe cha kisasa. Tulipiga gharama za chini kabisa za kuandaa ekari moja, tukaona mkulima lazima awe na milioni moja na laki mbili,” alisema.

Akaongeza: “Kwa mkulima mdogo wa Tanzania kiasi hiki ni kikubwa; anahitaji mkopo wenye masharti nafuu. Tuliwambia kwamba kwa sasa kimbilio lao ni TADB, na vikundi vyote viliazimia wataalamu wa TADB wavitembelee na kufanya tathimini yao wenyewe.”

Kampuni ya Lusitu AgroBusiness ndio imechochea ulimaji wa zao la parachichi na viazi mviringo mkoani Njombe na sasa imeanza ngwe ya aina hiyo mkoani Ruvuma ili zao la parachichi lilimwe kama zao la kimkakati kuinua uchumi wa wakulima wa mkoa huo na taifa kwa jumla.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, kampuni hiyo ilitangaza kwamba imewashawishi wakulima 200 kuunda vikundi 10 ili kulima kisasa zao la parachini kama zao la biashara mkoani Ruvuma mbali ya mahindi na maharage.

Mkakati wa kampuni hiyo unaungwa mkono na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (Sagcot) kwa maelezo kwamba, zao hilo lina soko la uhakika, hivyo litaboresha maisha ya wakulima.

Kampuni za Tanzanice na Pro-Organic zimesema ziko tayari kununua parachichi zitakazozalishwa Ruvuma na kuziuza barani Ulaya.

Mgaya alisema kampuni yake inaungana na wanavikundi katika kutafuta uwezeshaji wa TADB.

“Tunakubaliana na wakulima kwa sababu hoja zao ni za msingi. Wanataka kulima zao lenye soko la kudumu; wanunuzi wapo. Gharama za kulima zao hilo kwa eka ni kubwa kwa upande wao. Wenzetu wa TADB wakija tutashirikiana nao kuondoa changamoto hii. Hili jambo linawezekana,” alisema.

Alisema wakulima katika vikundi hivyo wameonesha wazi nia ya kulima zao hilo kwani kila mmoja amechangia Sh 105,000 ili apewe elimu ya kuandaa shamba, upimaji wa afya ya udongo, uandaaji wa miche na upandaji wa miche 100 katika ekari moja.