Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 11Article 562561

Habari za Biashara of Monday, 11 October 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wakulima walia na bei ya mbolea, pembejeo

Wakulima walia na bei ya mbolea, pembejeo Wakulima walia na bei ya mbolea, pembejeo

WAKULIMA mkoani Mbeya wameiomba serikali kutafuta namna ya kupunguza bei ya mbolea pamoja na pembejeo zingine ili kuwasaidia kuongeza uzalishaji na kupata tija zaidi.

Wananchi hao walitoa ombi hilo juzi wakati wa uzinduzi wa duka la pembejeo la kampuni ya ukopeshaji wa pembejeo ya One Acre Fund lililopo katika Kijiji cha Imezu Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kusema kwa sasa bei ya mbolea ipo juu kuliko miaka yote.

Mmoja wa wananchi hao, Joseph Mbuna alisema kwa sasa bei ya mbolea haiendani na ya mazao hali ambayo itasababisha wananchi kushindwa kumudu bei hizo na kushuka kwa uzalishaji wa mazao.

Alisema kwa sasa bei ya mbolea ni kuanzia Sh. 80,000 na kuendelea wakati ya mahindi ambayo yalivunwa msimu uliopita yanauzwa kwa bei ya kati ya Sh. 3,500 na 6,000 katika Mkoa wa Mbeya na kwamba ili mwananchi anunue mfuko wa mbolea atahitaji kuuza mahindi mengi.

“Mwaka huu bei ya mbolea imekuwa tatizo kubwa sana, itatufanya wakulima tusizalishe kabisa, tunaomba serikali itusaidie kukabiliana na tatizo hili,” alisema Mbuna.

Mwakilishi wa One Acre Fund wa mikoa ya Mbeya na Songwe, Erica Kafwimi, alisema waliamua kufungua duka hilo ili kuwarahisishia wakulima kupata mbolea na pembejeo zingine kwa wakati na kuondoa tatizo la wananchi kuuziwa pembejeo feki.

Alisema wamekuwa wakifanya kazi na wakulima kwa muda mrefu hasa kwenye ukopeshaji wa pembejeo za kilimo na kwamba kwa sasa wataendelea kuwahudumia wananchi wa maeneo yote ambayo wamekuwa wakiyahudumia.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kupunguza bei za mbolea ili wananchi wengi waendelee kutumia na kuongeza uzalishaji.

Alisema serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo la mfumuko wa bei ya mbolea ili wananchi waendelee kuzalisha kwa tija.