Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 10 12Article 562732

Habari za Biashara of Tuesday, 12 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wawekezaji EAC njooni Zanzibar- Dkt Mwinyi

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali  Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewaalika wawekezaji kutoka Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingine duniani kuja kuwekeza Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema hayo wakati akifunga Onesho la Kwanza la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoanza Oktoba 9, mwaka huu.

Alisema katika Visiwa vya Zanzibar kuna maeneo mengi ya uwekezaji hususan katika uchumi wa bluu kupitia bahari na maeneo mengine kama ya utalii wa kitamaduni.

Mwinyi alisema Tanzania kwa jumla kuna vivutio vingi vya utalii, hivyo wageni kutoka EAC na nchi mbalimbali duniani waje kuwekeza Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema katika nchi za EAC, pia kuna vivutio vingi vilivyopo karibu kila eneo, hivyo nchi hizo zifanye jitihada kuwavutia watalii wengi zaidi ili vivutio hivyo vichangie zaidi katika maendeleo ya nchi hizo.

"Ripoti ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) inaonesha kwamba, idadi ya watalii wanaokuja ni asilimia 8.6 ya watalii wote wanaokuja Bara la Afrika wakati idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.3 ya watalii wote duniani,” alisema.

Akaongeza: “Idadi hiyo ni ndogo kulingana na watalii wanaokuja Afrika hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza idadi ya watalii zaidi."

Alisisitiza jitahada zaidi kufanyika ili kuongeza idadi ya watalii hasa baada ya janga la Covid-19 kujitokeza na kwamba, licha ya janga lazima utalii na vivutio vyake utangazwe ili kuhakikisha watalii wengi zaidi wanakuja katika nchi za EAC zikiwamo Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kwa sasa mapato yanayotokana na utalii hayaendani na wingi na ubora wa vivutio vya utalii vilivyopo na akasema nchi za EAC ikiwamo Tanzania, zina utajiri wa vivutio vya utalii vikiwamo hasa vya asili.

Dk Mwinyi alizihimiza nchi za EAC kuboresha sera za utalii ili kusaidia wawekezaji katika sekta ya utalii kufanya kazi kwa ufanisi.

Alisema serikali inasisitizia uchumi wa bluu kwani zipo fursa za kuwekeza katika hoteli, meli za kitalii, michezo ya bahari na masuala mengine ya utalii na uchumi.

Alisema Zanzibar imefungua fursa nyingi za uwekezaji ukiwemo uvuvi katika bahari kuu, majengo, utafutaji wa mafuta na gesi na kusisitiza kuwa, Zanzibar ni njema na anayetaka aje.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro, alisisitiza kuwa, sekta ya utalii katika EAC, imeleta sura mpya kwa nchi hizo katika masuala ya utalii.

Alisema onesho kama hilo litafanyika mwakani nchini Burundi na kuwa, baada ya onesho hilo kumalizika jana, waoneshaji watapata fursa za kwenda kutembelea vivutio vya utalii vya hifadhi za taifa za Mkomazi, Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na vivutio vingine vya utalii vilivyopo Zanzibar.

Ndumbaro alisema onesho hilo limewashirikisha waoneshaji wakubwa wa bidhaa za utalii zaidi ya 100 huku waoneshaji 41 wakitoka katika nchi 19 za Afrika, Ulaya na Marekani. Nchi zote sita wanachama wa EAC zilishiriki na hivyo kufanya jumla ya nchi 25 zilizoshiriki.

Mkurugenzi Mkuu wa Forodha na Biashara wa EAC, Kenneth Bagamuhunda, alisema maonesho hayo yalipaswa kuanza mapema, hivyo kwa mwanzo huo mzuri unaonesha mwamko wa kuungana pamoja kwa nchi za EAC katika kutangaza utalii kwa kila nchi.