Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 28Article 560092

Habari za Biashara of Tuesday, 28 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Waziri Jafo aagiza makontena 45 yenye mifuko ya plastiki yateketezwe

Waziri Jafo aagiza makontena 45 yenye mifuko ya plastiki yateketezwe Waziri Jafo aagiza makontena 45 yenye mifuko ya plastiki yateketezwe

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, ametoa siku 45 kwa Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania bandarini, Florence Mniko, kuteketeza makontena matano yenye mifuko ya plastiki yaliyotelekezwa Bandari Kavu ya Ubungo, Dar es Salaam.

Alitoa maagizo hayo jana alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua makontena hayo kwenye Bandari Kavu ya Ubungo, kuwataka TRA, TPA na Baraza la Taifa ya Uhifadhi na Utunzaji Mazingira (NEMC) kushiriki kuteketeza mifuko hiyo ambayo imepigwa marufuku kutumika hapa nchini.

Makontena hayo yalikuwa yanasafirishwa kuelekea nchini Malawi lakini yamekaa bandarini kwa zaidi ya mwaka mmoja.

"Nawapa siku 45 kuteketeza mifuko hii chini ya usimamizi wa NEMC na baada ya hapo naomba nipate ripoti yake, hawa waliotelekeza makontena haya wana mbinu nyingi na wanazunguka sana maofisini, sasa jambo hili nimelifunga rasmi na natoa hizo siku 45 kuteketeza mifuko hii," alisema Jafo.

Meneja wa TRA Bandarini, Mniko, alisema makontena hayo yalikuwa safarini kwenda Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yalikaa bandarini zaidi ya siku 21 zinazoruhusiwa kisheria, lakini baadaye yalitelekezwa na waagizaji wa makontena hayo," alisema Mniko.

Alisema sheria ya nchi hairuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki, TRA haiwezi kuuza mizigo kwenye kontena hivyo sasa njia pekee ni kuyateketeza.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEMC, Bernad Kongola, alisema kuwa makontena hayo yapo matano na yalikuwa njiani kuelekea Malawi.

"Tulipata taarifa kuna watu walitaka kununua mizigo hii, lakini sheria yetu iliyoanza kutumika Juni 2019 inapiga marufuku uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, lakini sheria hii ipo kimya aielezei juu ya jambo kama hili la kupitisha bidhaa hizi zilizopigwa marufuku matumizi yake hapa nchini, sasa hawa wametelekeza hivyo serikali itachukua hatua ya kuteketeza," alisema.

Serikali ilipitisha sheria ya kupiga marufuku uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki Juni, mwaka 2019, ili kutunza mazingira baada ya kuonekana mifuko hiyo inachafua kwa kiasi kikubwa mazingira.