Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 17Article 543151

Habari za Biashara of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara ya Mawasiliano inavyojipanga kukuza uchumi

Wizara ya Mawasiliano inavyojipanga kukuza uchumi Wizara ya Mawasiliano inavyojipanga kukuza uchumi

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imejipanga iwe moja ya njia kuu ya kukuza uchumi wa kisasa unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Faustine Ndugulile akizungumza jijini Dodoma jana, alisema inataka kuona sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari iwe na mchango mkubwa kwenye kuongeza pato la nchi.

"Katika njia kuu za uchumi ndani ya nchi yetu sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari ni mojawapo, sio wizara ya mabando na vifurushi peke yake, ni wizara ambayo inakwenda kuibadilisha hii nchi na kuisogeza katika uchumi wa kidijitali," alisema.

Alisema wizara hiyo inagusa kila sekta ndani ya serikali hivyo itaiwezesha nchi kujenga uchumi huo na ndani ya miaka mitano kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kisheria, kisera na kimifumo ili kuendana na kasi ya mabadiliko duniani.

Dk Ndugulile alisema hayo wakati akifungua mkutano kati ya wizara hiyo na wahariri wa vyombo vya habari na wadau wa wizara hiyo.

"Sasa hivi dunia inaongelea mapinduzi ya nne ya viwanda yanayohusu mabadiliko ya kiuchumi, ambapo sasa hivi Tehama itakuwa na nafasi kubwa katika shughuli mbalimbali ambazo tutakuwa tunazifanya," alisema.

Alisema Tanzania lazima ijipange na kujiandaa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili kujenga uchumi wa kidijitali, pamoja na kuimarisha biashara mtandaoni.

"Ukiangalia trend (mwenendo) ya biashara sasa hivi ndani ya nchi yetu na hususani biashara za vijana mtaona zimebadilika sana. Vijana wanaagiza mzigo wao iwe ni nje ya nchi au hapa ndani ya nchi anaweka mzigo wake nyumbani, anapiga picha zake nzuri, anaingia instagram, twitter, facebook anapost picha zake, wewe mteja ukipenda kile kitu mtapatana bei inbox, atamtuma bodaboda atakuletea bidhaa yako nyumbani," alisema.

Alisema lazima uwekwe mfumo wezeshi ili kukuza biashara mtandao ya kuwezesha shughuli za serikali zifanyike kidijitali.

"Tunataka sasa hivi serikali iende katika kiganja cha mwananchi. Tunataka tutumie Tehama, sisi kama serikali tumeona hii ni njia mojawapo kuanza kuongeza ufanisi, kuongeza tija na uwajibikaji ndani ya serikali," alisema.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Kundo Mathew alisema serikali inajiweka tayari kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani na kwamba vyombo vya habari ni wadau muhimu kufikisha taarifa kwa wananchi.