Uko hapa: NyumbaniHabariDiaspora2021 06 11Article 542167

Diasporian News of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wizara yatoa ufafanuzi wastaafu wa Zanzibar

Wizara yatoa ufafanuzi wastaafu wa Zanzibar Wizara yatoa ufafanuzi wastaafu wa Zanzibar

MASUALA ya wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano (SMT) wanaoishi Zanzibar yanashughulikiwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Fedha na Mipango ya Muungano na Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar.

Ufafanuzi huo ulitolewa bungeni Dodoma jana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yusufu Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan Omari (King) wa CCM.

Mbunge huyo alitaka kujua, serikali ina mpango gani wa kufungua ofisi ndogo ya Hazina Zanzibar kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Muungano ili kurahisisha huduma kwa wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wanaoishi Zanzibar.

Akijibu, Masauni alisema: “Kwa wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoishi Zanzibar, Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) mara zote imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kuwahudumia.”

“Wanafanyakazi kwa ushirikiano katika kupokea hoja za madai ya wastaafu hao na kuziwasilisha Hazina Makao Makuu - Dodoma kwa ajili ya taratibu za malipo,” alisema.

Masauni alisema Wizara ya Fedha na Mipango ya SMT itaendelea kuimarisha ushirikiano na Wizara ya Fedha na Mipango ya SMZ katika kuwahudumia wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wanaoishi Zanzibar kama ambavyo hushirikiana na Ofisi za Hazina ndogo zilizopo Tanzania Bara.

Alisema huduma za malipo ya mafao ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango hufanyika kupitia Ofisi za Hazina Makao Makuu, Dodoma.

Aidha, alisema Ofisi za Hazina ndogo zilizopo katika mikoa ya Tanzania Bara hutumika kwa ajili ya kukusanya hoja za wastaafu na kuziwasilisha Hazina Makao Makuu, Dodoma.

Join our Newsletter