Uko hapa: NyumbaniBurudani2021 10 04Article 561133

Burudani of Monday, 4 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Hii ndio sababu ya Mac Voice kushindwa kusoma

Mwimbaji Mac Voice Mwimbaji Mac Voice

MSANII wa muziki wa kizazi kipya Mac Voice amesema hakupenda kuacha shule ila aliona anampa shida mama yake kumsomesha wakati hakuwa na uwezo.

Akizungumza na gazeti hili jana, msanii huyo ambaye yupo chini ya lebo ya Next Level Music (NLM) inayoongozwa na msanii, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ alisema aliishia kidato cha kwanza baada ya kuona mama yake hana uwezo wa kumsomesha.

"Sikupenda kuacha shule, lakini nilihisi namtesa mama kwa sababu alikuwa anapata shida kunisomesha kwa kuwa alikuwa na uwezo mdogo, niliishia kidato cha kwanza,” alisema

Alisema anamshukuru Chege Chigunda kwani ndiye mtu wa kwanza kumsaidia akafanikiwa kuachia nyimbo mbalimbali kama Teamo Remix na Bamba ambazo zinaendelea kufanya vizuri.

“Mimi nilitoa ngoma nikawa napeleka vituoni vya redio, yaani kiufupi nilikuwa napeleka ngoma redio zote na mara ya mwisho Chege alinicheki na kuniambia anaipenda sana,” alisema.

Mac Voice mzaliwa wa Bagamoyo, Pwani alisema anashangaa watu wanaosema ana sauti inayorandana na ya Rayvanny na anadhani kwa sababu bado ni mpya masikioni mwao, lakini wakiendelea kumsikiliza wataona tofauti.

Rayvanny alimtambulisha Mac Voice kuwa msanii wa kwanza kwenye lebo yake Septemba 24, mwaka huu.