Uko hapa: NyumbaniBurudani2021 10 10Article 562348

Televisheni of Sunday, 10 October 2021

Chanzo: Mwananchi

Menina aidai Dstv fidia ya Sh1.1 bilioni

Menina aidai Dstv fidia ya Sh1.1 bilioni Menina aidai Dstv fidia ya Sh1.1 bilioni

Msanii wa kike Tanzania, Menina Abdulkarimu Atiki ameiburuza mahakamani kampuni ya maudhui ya runinga kupitia ving’amuzi vya DSTv MultiChoice South Africa na mbia wake nchini Tanzania, MultiChoice Tanzania akiidai fidia ya Sh1.12 bilioni kwa madai ya kumkashifu.

Menina ambaye pia ni mwigizaji, mshereheshaji na balozi wa bidhaa ameishtaki kampuni hiyo ya Afrika Kusini inayofanya biashara zake katika nchi mbalimbali za Afrika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiwakilishwa na wakili, John Mallya.

Wengine katika kesi hiyo ni mhariri wa kipindi cha ICU- Chumba cha Umbea kupitia chaneli ya Maisha Magic Bongo kinachosimamiwa na MaultiChoice Tanzania. Watangazaji wa kipindi hicho ni Maimartha Jesse, Juma Lokole na Kwisa Thompsn maarufu Kamanda Mzee Mkavu.

Katika hati ya madai ya kesi hiyo namba 133 ya mwaka 2021, msanii huyo anadai kuwa wadaiwa hao walimkashifu kutokana na maudhui waliyoyarusha Julai 23, 2021 katika kipindi hicho kuhusu na kifo cha mumewe.

Menina anaeleza kuwa mumewe alifariki dunia Julai 19, 2021, familia yake na ya mumewe zilikubaliana maziko yafanyike Mtoni kwa Aziz Ali, nyumbani kwa shangazi wa marehemu, Mariam Kihiyo.

Amedai kuwa wakati mazishi yakiendelea, Maimartha, Lokole na Kwisa waliwahoji majirani wa shangazi wa marehemu kwa nia ovu walipenyeza maneno yaliyowachochea kutoa maneno kuonyesha kuwa hakuwa na upendo kwa mumewe, huruma wala maadili.

“Hata kumhudumia alikuwa hafanyi wakati anaumwa (alipokuwa amelazwa hospitali ya Temeke), alikuwa hamuangalii mume wake, wala hakuwa anamsafisha."

“Tangu ndugu yetu anaumwa mpaka sasa sura yake hatuioni (Menina huyo), ana roho mbaya kama mchawi..., ndio hajaja hata siku moja kwa mume wake, katuulia mtoto wetu inatuuma sana, kahusika, akamle nyama , tumechoka na mambo yake, tumechoka, anatembelea nyota, wasanii wachawi."

Maneno mengine anayoyalalamikia Menina ni yale yaliyotamkwa na Maimartha na Kwisa, "…we unavyomuona Menina anaweza? Ataweza kwani ameshaanza hiyo eda yenyewe…, hata msibani hajafika, hata msibani hajafika."

Amedai kuwa alipata madhara ya kiakili na maumivu ya kisaikolojia kwani ICU- Chumba cha Umbea ni moja ya kipindi maarufu kinachorushwa nchini, Afrika Mashariki na katika nchi zote zinazozungumza lugha ya Kiswahili.

Menina amedai kuwa shughuli zake za ubalozi wa bidhaa, muziki, filamu na ushereheshaji zinahitaji kudumisha sifa njema kulinda jina na heshima na kwamba itamchukua takribani miaka mitano kusafisha jina na heshima yake, hivyo ataathirika kwa kupoteza kipato kikubwa ambacho amekuwa akikipata kwa shughuli hizo.

Amefafanua kuwa katika ubalozi wa bidhaa analipwa Sh1.5 milioni kwa mwezi na mwaka 2020 alijipatia Sh180 milioni, hivyo kwa miaka hiyo mitatu atapoteza kipato cha jumla ya Sh540 milioni .

Katika muziki na uigizaji anadai kuwa anaingiza Sh50 milioni kwa mwaka, kama ilivyokuwa kwa mwaka 2020 na hivyo kwa miaka mitatu atapata hasara ya kupoteza kipato cha jumla ya Sh150 milioni.

Katika ushereheshaji amedai kila wiki kwa mwaka 2020 alijipatia Sh144 milioni na kwamba kwa miaka mitatu atapoteza Sh432 milioni, huku akidai kuwa tayari wateja wake 24 wameshafuta oda zao kwake.

Pia amedai kuwa kwa kashfa hiyo amepoteza heshima kama mama wa watoto wawili, kama mwanajamii kwa jumla na kama muumini wa dini ya Kiislamu.

Pamoja na fidia hiyo, pia Menina ameiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu kwa wadaiwa, mawakala wao, waajiriwa na mtu au kundi la watu lenye kudai kuwa na maslahi nao kutokumkashifu kwa namna iwayo yoyote ile.

Pia anaomba fidia ya madhara ya jumla na malipo ya adhabu ya madhara kwa kadiri mahakama itakavyopima kutokana na athari za maudhui hayo ya kashfa.

Vilevile riba ya asilimia 12 kwa mwaka kutoka tarehe ya hukumu hiyo mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote na gharama za kesi.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Amir Mruma ilitajwa kwa mara ya kwanza Septemba 27, 2021, lakini MultiChoice South Africa haikuwepo na Jaji Mruma aliamuru ipelekwe tena hati ya wito na akaahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, 2021