Uko hapa: NyumbaniBurudani2019 11 12Article 487501

Burudani of Tuesday, 12 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Ndani ya boksi: Hilo limeisha, kuna lingine? Twenzetu Wasafi Festival

Ndani ya boksi: Hilo limeisha, kuna lingine? Twenzetu Wasafi Festival Ndani ya boksi: Hilo limeisha, kuna lingine? Twenzetu Wasafi Festival

Diamond Platnumz. Nyota yake kimataifa ilianzia kwenye shughuli kubwa kama ya leo. Wakakutana na mkali Davido, wakabonga, wakaelewana.

Fasta kama treni la umeme, wakagonga remix ya Number One. Boonge moja la ngoma ambalo liliifunika kabisa ile Number One halisi. Davido alionyesha utofauti wake.

“Tupate ubaridi kidogo tukale na ugali wa muhogo, All I want is a bottle of moet, oh wey... Baby we can do in your way, Anything you want it’s okay, All I want is a bottle of moet, for you... Tanzania to Lagos, I go make you famous...”

Mistari michache ya dogo tajiri la sanaa toka Lagos. Ilipindua meza ya goma la Mondi na kuonekana kitu kipya.

Hii ndo maana halisi ya kupiga ngoma na msanii mkubwa. Siyo unagonga ngoma na mtu wa nje watu wanaanza kuona bora ungefanya peke yako. Na ukitaka kujua ‘huu izi’ Davido? Tazama ngoma zilizofuata za Mondi baada yake, alizofanya na wasanii wa nje hazijafikia ‘piki’ ile ya Number One remix. Davido alivuka viwango vya goma ‘orijino’. Kuna Mr Flavour na Nana. Morgan Heritage na Hallelujah. Kuna P Square na Kidogo. Kuna Fire na Yemi Alade. Wakawaka na Rick Ross. Usisahau Ne-Yo na Marry You. Hawa wote wakubwa sana kimuziki duniani. Lakini bado Davido, siyo kwa kuwa wa kwanza kufanya naye kimataifa, ila lile dude lilimsafirisha mbali sana Mondi.

Zingatia sana neno “Tanzania to Lagos, I go make you famous...” Alimaanisha huyu mwamba wa Kipopo. Kwani wengine waliofuata walifanya ngoma mpya kabisa na Dai. Lakini Davido aligonga naye ngoma kubwa ambayo tayari ilishasambaa kote. Lakini akafunika na kuifuta kikatili kabisa ile ngoma ‘orijino’ yake. Na kumpaisha zaidi.

Kulikuwa na kelele za dem mmoja (simkumbuki jina). Akidai ile ‘biti’ ya Number One, Mondi aliiba toka kwake. Ila baada ya ule mdude na Davido kelele zilitoweka kama mbavu zenye mafuta kwenye mwili wa Chid Beenz. Toka hapo dogo akapaa ghafla kama maranda ya mbao kwenye upepo mkali. Akawa mkubwa.

Kikubwa ni kwamba juhudi binafsi za Mondi zilichangia kuwa hapa alipo. Nafasi hii aliipata Alikiba kwa kugonga ngoma moja na R Kelly wakati ule. Na kwenye ngoma ile kulikuwa na nyota kibao wa muziki duniani na Afrika lakini Kiba hakuitumia fursa hiyo hata kwa Chameleone wa Uganda. Hata mwamko wa fikra kwetu sote ulikuwa bado sana.

Mondi hakurudi Sinza kuendelea kucheza marede. Akaendelea kusaka ‘koneksheni’ zaidi. Na hapa ndipo utaona umaalumu wa ‘Mendez’ Sallam ndani ya WCB. Hiki ndio kitengo chake yule mtoto wa Kiluguru. Na kwa macho tu bila kutumia majini utaona kafanya jukumu lake kwa kiwango cha juu.

Ngoma alizoendelea kufanya na wasanii wakubwa kimataifa zilikuwa na maana kubwa kwa sanaa yake. Hata kama Mwananyamala, Kimara, Simanjiro, Uyui na Kamanga Ferry huko Mwanza masikio yao hayakujenga upendo nazo. Dunia ya kwanza ya wenzetu ilizidi kumjenga. Hili ndo bao kubwa la Mondi kisanaa.

Na ieleweke pesa nyingi za muziki kwa sasa zipo YouTube. Wimbo ambao yupo Ne Yo, Rick Ross, Morgan Heritage, P Square, Mr Flavour na wengineo wa aina ile lazima utapata watazamaji wengi YouTube, kutokana na ukubwa wa majina yao.

Leo hii kuna tamasha kama lile lililofanya Mondi akutane na Davido. Na mhusika mkuu ni Diamond. Leo ni Wasafi Festival. Wanamuziki kibao wa nje na ndani wapo kukinukisha. Mungu awape nini wanamuziki wetu? Mnaenda kwenye shughuli iliyoandaliwa na mtu ambaye mafanikio yake yalianzia kwenye shughuli kama hiyo.

Mmejiandaaje? Unadhani Ferouz utafanya kitu cha tofauti na WizKid jukwaani? Kiasi cha mchizi huyo wa Kinaija aombe ‘kolabo’ na wewe mfanye ngoma? Au wewe ndo unatakiwa ujiandae kwa ‘koneksheni’ na WizKid? Achana na ‘kolabo’ inaweza kuwa utata kwa kuwa mko wengi, hata ‘koneksheni’?

Unadhani Chid Benz Wasafi Festival ni jukwaa la kuonyesha umerudi kwenye mstari? Au ni wakati wa muunganiko wa sauti yako na wasanii wa kimataifa. Au muunganiko wa maongezi ya kupeana michongo zaidi? Walikuja kina Jah Rule, 50 Cent, Shaggy, Luda Criss na wenzao ukiwa juu kama Mlima Kilimanjaro.Hukuweza kufanya kitu zaidi ya kuimbisha watu jukwaani na kurudi Ilala. Mlitazamana na kina Kalapina kishindani. Kwa maana kuwa wakati wenzenu wanatanua muziki wao nyinyi mlikuwa ‘bize’ na neno Bongofleva na Hip Hop. Hamkuona umuhimu wa ujio wa kina Lil Kim, Fat Joe, Bennie Man wala Sean Paul. Mkaishia kulewa nao Bar One Masaki enzi hizo.

Vita ya Bongofleva ‘wabana pua’ na Hip Hop ‘wagumu’ mliibebea bango kama majuha. Mkawa hata hamuelewi mnaongea na mnataka nini. Leo hii mwana Hip Hop Rick Ross anagonga ngoma na Mondi anapita na ‘biti’ zenu za Afro Beat na P Square kama hana akili nzuri.

Mwanzoni walianza kutengeneza kwa neno rap katuni za kina Nature na Hip Hop za kina Jay Mo. Baadaye ikawa vita ya wabana pua kina Ruta Bushoke na ngoma ngumu kina Fid Q. Ikaanza Bongofleva na Hip Hop. Aliyeimba ni Bongofleva, aliyechana Hip Hop. Na waimbaji walitengwa na watu wa Hip Hop. Upuuzi.

Mwisho ikawa neno Bongofleva kama kitu cha kishamba hivi. Na Hip Hop likawa kama neno la waliofeli kimaisha. Haya yote yalikuja mwanzoni mwa miaka ya 2000. Maneno yakawa mengi badala ya kazi bora.

Kuna wakati watoto wa Arusha waliaminisha umma kuwa Hip Hop ipo kwao. Nenda Arusha leo kisha anzia klabu mpaka kwenye daladala husikii walichotaka kutuaminisha mwanzoni hata wasanii wengi wa huko wanafanya muziki biashara kuliko Wamachinga. Zilikuwa kelele za njaa njaa tu. Kizazi cha Diamond ndicho kilichovunja hili daraja.

Tatizo kapitiliza zaidi kwa kuua hata neno Bongofleva lenyewe na Hip Hop sehemu kubwa anajulikana yeye na WCB kuliko aina ya muziki wetu na neno Bongofleva. Zamani hata majirani zetu walilitamani neno hilo. Bongofleva ulikuwa ni utambulisho wa muziki wetu. Kuanzia kwenye majarida makubwa, runinga maarufu na mitandaoni. Muziki wetu utambulisho wake ulikuwa huo na ulitaka kuteka muziki, wimbo wowote wa Kiswahili uitwe Bongo fleva.

Ni vigumu leo Mondi kutajwa kama mwanamuziki wa Bongofleva. Jukwaani, runingani, gazetini au popote ndani na nje ya nchi. Jina la Bongofleva linatoweka kama sharafa za Profesa Mussa Assad kwenye ofisi za CAG. Anatajwa kwa jina lake, lakini Wanaijeria bado ile Naija wameishikilia.

Hivi karibuni nilitazama runinga nikaona kituo cha burudani cha Trace, kimeanzisha kitu kinaitwa ‘Trace Naija’ na ‘Trace Mziki’. Hii inahusu ngoma za Afrika Mashariki. ‘Trace Naija’ inahusu Wanaijeria. Naamini ingekuwa nyakati zile za ubora ingeitwa ‘Trace Bongofleva’.

Tulikuwa wakubwa kwa kutumia neno hili ikijumuisha muziki wote wa Tanzania na Afrika Mashariki. Sasa tumekuwa ‘andadogi’ kwa kumtegemea staa mmoja tu Mondi. Naija walikuwa wakituogopa katikati ya miaka ya 2000. Leo hii ukitaka kutusua kimuziki eti lazima umshirikishe Mnaijeria. Wakati kina Jide wakienda kwenye tuzo nyakati zile mahotelini walipishana na Wakongo na ‘Wasauzi’ kina Brenda Fassie. Leo mwaka wa 10, Wanaijeria wakienda kwenye tuzo popote duniani koridoni na vibaraza vya hotelini, wanapishana na Mondi miaka yote. Kwa nini asitambulike yeye na si Bongofleva?

Vita vya rap katuni na Hip Hop halisi? Imetoweka. Wabana pua na Hip Hop? Kwisheni. Bongo Fleva na Hip Hop? Hakunaga. Kuna lingine?

Team Kiba na Team WCB? Hilo limeisha, twenzetu Wasafi Festival. Ni mwendo wa kutupia pamba kali, keshi mfukoni na totoz za geti au za kona. Maisha bora ni yenye kitu kipya zaidi. Na hiki ni kipya.